Licha ya keki kuwa miongoni mwa vitu muhimu vinavyotumika katika matukio mbalimbali ya kijamii kama harusi, siku za kuzaliwa, ubatizo na sherehe nyingine nyingi, bado jamii haijaipa kipaumbele na thamani inayostahili.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Moro Bakers Cake Picnic Diana Erasto, katika tukio lililowakutanisha waokaji wa keki mkoani Morogoro. Amesema kuwa keki si tu mapambo ya sherehe, bali pia ni sanaa na fursa ya kiuchumi inayoweza kubadili maisha ya watu, hususan vijana na wanawake tunapaswa kuipa keki heshima yake kama tunavyofanya kwa bidhaa nyingine muhimu kwenye maisha yetu ya kila siku.

Kwa upande wake, Nuwayla Mohamed, muokaji chipukizi wa keki, amewashauri wazazi kuanza kuwajengea watoto misingi ya ujasiriamali mapema kwa kuwahusisha katika shughuli kama uokaji wa keki. Amesema watoto wengi wana vipaji lakini havikui kutokana na kukosa msaada wa awali kutoka kwa wazazi, akibainisha kuwa ujasiriamali unaweza kuwa msingi mzuri wa maisha yao ya baadaye.
Naye Afisa Masoko wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi, Goodluck Kway, amesema kuwa kiwanda hicho kimejipanga kuwasaidia waokaji kwa kuzalisha aina maalum ya sukari yenye ubora wa juu, inayokidhi mahitaji ya uokaji.