Msafara wa wataalamu kutoka Jiji la Chengdu mkoa wa Schuan nchini China umetembelea Halmashauri ya jiji la Dar es salaam ili kuanzisha mahusiano mbalimbali yakiwemo ya kibiashara, elimu, kilimo nk.
Ugeni huo ulioongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Chengdu na Naibu Meya, Bw. Wang Pingjiang ambapo ulipokelewa na Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo na Mkurugenzi wa Jiji Elihuruma Mabelya.
Katika mazungumzo yao yaliyotumia takribani saa mbili, ujumbe wa wataalamu hao kutoka Jiji hilo la nne kwa ukubwa nchini China walionesha kuvutiwa na namna Jiji la Dar es salaam linavyoendelea kwa kasi katika miundombinu.
‘Hii ni mara yetu ya kwanza kufika Tanzania na imekuwa bahati katika nchi zote za Afrika, tunatembelea katika majiji mawili tu mojawapo ni hili la Dar e salaam’. Alisema Bw. Pingjiang
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema ushiriano baina ya nchi hizi mbili uliasisiwa na viongozi wakuu Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kiongozi wa Taifa la China Mao Tse – Tung hivyo hawana budi kuuendeleza.
” Tunawajibu kuwa na mahusiano kati ya miji mikubwa Tanzania na China ili kuenzi mahusiano mazuri kati ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Xi Jinping waliorithi kutoka kwa waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Mwl. Nyerere na Mao Tse-Tung”.Alisema Mpogolo
Mkurugenzi wa Jiji hili Elihuruma Mabelya ameainisha maeneo ambayo angependa washirikiane nao katika kubadilishana ujuzi kuwa ni Elimu, Uwekezaji, Utunzaji wa Mazingira na miundombinu.
Katika kikao hicho pande hizo mbili zimekubaliana kuanza mchakato wa kuelekea kuwa na makubaliano rasmi ya ushirikiano ambao utafuata taratibu zote za kiserikali.
Jiji la Chengdu ni moja ya majiji makubwa nchini China ambapo mpaka kufikia mwaka 2023 ilikadiriwa kuwa na wakazi milioni 21 ambapo ni kitovu cha uchumi, teknolojia, fedha, na miundombinu ya usafiri likiwa na viwanja viwili vya ndege vya kimataifa,Viwanja viwili 2 vya ndege, zaidi ya vyuo vikuu 51,na eneo la Mji wa mfano uliokuwa kwa kasi zaidi duniani.