Na; mwandishi wetu
Kesi ya kupinga uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume Huru ya kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini Oktoba 29 mwaka huu na siku zilizofuata iliyofunguliwa na Watanzania watatu (3) wakiongozwa na Mwanaharakati Rosemary Mwakitwange imetajwa leo, Jumanne Desemba 02.2025 kwa mara ya kwanza kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Hussein Salum Mtembwa
Kesi hiyo ambayo leo imeendesshwa kwa mtandao, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye ni mjibu maombi wa kwanza amewakilishwa na Mawakili wa Serikali wawili (2) ambao ni Mark Mlwambo na Stanley Kalokola, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambao ni wajibu maombi wa 10 wamewakilishwa na Wakili Ferdinand Makore, na wajibu maombi wa pili hadi wa tisa (9) ambao kimsingi wote ni Wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman hawakuwepo Mahakamani kutokana na kwamba hawana taarifa (hawajawa served), hivyo Mahakama kutoa siku mbili (2) kuanzia leo kwa upande wa waleta maombi kuhakikisha wanawafikishia taarifa hiyo
Wakili wa Serikali Mkuu Mark Mlwambo akaomba siku 10 za kuwasilisha kiapo kinzani ombi ambalo halikukubaliwa na Mahakama badala yake, Mahakama ikatoa siku saba (7) kwa wajibu maombi wote wawe wamewasilisha viapo vyao kinzani Mahakamani, hiyo ni hadi kufikia Desemba 09 mwaka huu, na hivyo kesi hiyo kuhairishwa hadi Desemba 10 mwaka huu itakapotajwa tena Mahakamani, ambapo wahusika wote watafika Mahakamani moja kwa moja,
Kando ya Mwanaharakati Rosemary Mwakitwange, waleta maombi wengine kwenye kesi hiyo ni Mawakili Edward Heche na Deogratius Mahinyila ambao leo wamewakilishwa na Mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, lakini katika jopo hilo poa yupo Wakili Jebra Kambole

Imeelezwa kuwa Watanzania hao wamefungua kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake tisa (9) wakipinga uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Tume Huru ya kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini Oktoba 29 mwaka huu na siku zilizofuata, wakidai kuwa uamuzi huo si sahihi, si wa haki, na haukubaliki kutokana na sababu tatu (3) tofauti walizoainisha

Waleta maombi wanadai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya maamuzi ambayo si ya busara katika uundaji wa tume hiyo kutokana na kile walichodai kuwa madhumuni ya tume hayaeleweki na yanapotosha
Sambamba na hilo wanasema tume hiyo inaundwa na waliokuwa viongozi na watumishi waandamizi wa serikali (wazee wastaafu)
Wanasema tume hiyo ambayo kimsingi imenza rasmi kufanya kazi zake inakosa nguvu na mashiko kutokana na uhalisia uliopo kwa jamii, kwakuwa imeundwa kwa hali isiyoeleweka, na kwamba badala ya kushughulikia mauaji ya raia, kupotea kwa watu, mateso na ukiukwaji wa Katiba, badala yake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza madhumuni ya kuundwa kwake ni kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani, jambo ambalo wao wanaona kama vile matokeo yote ya vurugu hizo yamedharauliwa

Zaidi ya hayo, waleta maombi wanadai kuwa Tume hiyo imeundwa na waliokuwa viongozi na watumishi wastaafu bila kujumuisha waathiriwa wa vurugu hizo ambao wengi wao ni vijana (Gen-Z), Wawakilishi wa Vijana, Asasi za Kiraia (AZAKI), Mashirika ya Kidini na Taaluma ya Sheria, licha ya kuhusika na kuwa na maslahi ya moja kwa moja katika matukio hayo
“Watu walewale ambao hapo awali walihudumu katika Tume ya Marekebisho ya Haki Jinai ya mwaka 2023 ambayo haikutekelezwa, wameteuliwa tena, na kuunda muuondo wa tume unaweza kutabirika na usiokuwa na usawa, uteuzi wa aina hiyo hauwezi kuacha kufanya upendeleo, kuacha maslahi ya umma na katu hauwezi kutazama hali halisi ya kisasa” -imeeleza Hati ya Mashtaka
Aidha, imeelezwa kuwa mamlaka ya uteuzi imekiuka Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, katika vipengele kadhaa vya lazima ambavyo ni:
(i) Rais ameunda ‘Tume Huru ya Uchunguzi’, neno ambalo halipo popote katika Sheria, na kuifanya Tume kuwa chombo kisichojulikana kisheria,
(ii) Sheria inahitaji ufichuzi wa wazi wa madhumuni na uchapishaji kupitia Tangazo la Gazette, lakini Tume hiyo haikutangazwa kwenye Gazette la Serikali, na madhumuni yake hayakuwekwa wazi, na
(iii) Wajumbe wa Tume hawajala kiapo cha kisheria, na hivyo kufanya uteuzi wao kuwa pungufu na batili, pia kanuni za haki asilia za Kikatiba zilikiukwa
“Watu ambao taasisi zao, Ofisi au vitendo vyao vinahusishwa katika vurugu kama vile aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambaye ni mshtakiwa wa tisa (9) kwenye kesi hii, IGP wa zamani (mshtakiwa wa saba), na Majaji Wakuu wa zamani ambao ni washtakiwa wa pili na tatu, wote na wengine wameteuliwa kuchunguza masuala ambayo wanaweza kuhusishwa moja kwa moja wao wenyewe au taasisi walizokuwa wanaziongoza au kuzitumikia, hatua hii inavunja Sheria ya Haki ya Asilia ‘nemo judex in causa suas’ yaani huwezi kuwa Hakimu kwenye kesi yako mwenyewe” -imeeleza Hati ya Mashtaka
Aidha, Waleta maombi wanadai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameunda Tume hiyo kwa sababu zisizo sahihi, kwani amefanya hivyo ili kuziwahi tume za uchunguzi za Kimataifa, ametoa majibu ya uchunguzi hata kabla ya uchunguzi wenyewe haujaanza, ameteua watu watiifu kwake na kwa Marais walipita
Wanadai, pia kitendo cha kutumia lugha ya ‘uvunjifu wa amani’ inapunguza au kuondoa ukweli kuhusu suala la mauaji, kutokana na kile wanachosema kwamba rekodi inaonesha kwamba Tume hiyo imeundwa si kwa lengo la kufichua ukweli, bali kudhibiti simulizi, kulinda chama tawala (CCM), na kukwepa uchunguzi wa awali wa kimataifa
“Katika hotuba yake Rais alitoa lawama waziwazi, akidai kwamba vijana ‘walilipwa’, kwamba vyama vya upinzani vilichochea machafuko, na kwamba NGO’s na watendaji wa kigeni walishawishi matukio kabla ya uchunguzi wowote kuanza, kitendo cha kutoa hitimisho kabla ushahidi haujakusanywa ni kitendo cha uovu, pia alikiri kuunda Tume kuchukua hatua kabla ya vyombo vya uchunguzi vya nje havijaanza kutafuta ukweli, akionesha nia ya kubatilisha maswali mengine yanayoaminika, sambamba na uteuzi wa makusudi wa watu wenye migogoro, na watifuu kwa kwake au kwa Marais waliopita” -imeeleza Hati ya Mashtaka
Pia, Waleta maombi wanadai kuwa uamuzi huo unaonesha nia ya serikali ya kutofichua ukweli, kutokana na kile wanachoamini kwamba Tume hiyo inaweza kuendeshwa na iko kwaajili ya kujilinda, na kwamba haizingatii maslahi ya umma, badala yake wanadai kuwa ipo kwaajili ya kuilinda serikali na chama tawala (CCM) na si kutafuta ukweli
Waleta maombi wameendelea kusisitiza kuwa Tume hiyo haina maslahi yoyote iwa umma, kwakuwa haikuundwa kwa mujibu wa sheria, na imeundwa kwa nia iliyofichwa, na kwamba kwa sababu hizo wanaiomba Mahakama isimamishe Tume kufanya kazi na kuruhusu uchunguzi sahihi, wa kisheria, haki na huru uundwe
Sambamba na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni pamoja na Wajumbe wote wa Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini Oktoba 29 mwaka huu na siku zilizofuata ambao ni Mohamed Chande Othman, Ibrahim Hamis Juma, Ombeni Yohana Sefue, Radhia Msuya, Paul Meela, Said Ally Mwema, Balozi David Kapya, Stargomena Lawrence Tax, sambamba na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).