Latest Posts

KIDATA AANDALIWA ZENGWE MGOMO WA WAFANYABIASHARA

Inatajwa kuwa tuhuma zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuhusisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata ni za kughushi, na zinazolenga kumchonganisha kiongozi huyo na mamlaka ya uteuzi ili aondolewe kwenye nafasi hiyo, na kutoa mianya kwa ‘genge’ la wakwepa kodi, wala rushwa na wote wasiolitakia mema Taifa ‘kuchomeka’ mtu wao.

Jambo TV imeshuhudia mijadala mbalimbali inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa TRA chini ya Kidata imekuwa ‘mwiba’ mchungu kwa wafanyabiashara nchini kwa kile kinachotajwa kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikitoa makadirio ya kodi yasiyoendana na uhalisia, ubabe na kutosikiliza hoja za wafanyabiashara ambao kimsingi ni walipa kodi wakubwa nchini, hilo likienda sambamba na ujumbe unaoshinikiza kiongozi huyo ajiuzulu au aondolewe ili apatikane mtu mwingine anayetajwa kuwa atakuwa rafiki kushughulikia matatizo ya wafanyabiashara nchini.

Hata hivyo taarifa za ndani na za kuaminika kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo serikalini zinadai kuwa Kidata amekuwa kinara wa kusimamia sheria zinazotungwa na Bunge, kutocheka na wazembe, wakwepa kodi na wala rushwa kwa namna yoyote ile jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limefanikisha kuziba mianya ya wajanja wajanja waliokuwa wanatumia ‘kichaka’ cha TRA kufanya ‘uhuni’ usiolisaidia Taifa kwa muda mrefu.

Takwimu za haraka zinaonesha kuwa TRA chini ya Kidata imekuwa ikipaisha ukusanyaji wa mapato kila uchwao jambo ambalo ni jema kwa Taifa, mfano mwezi Desemba 2023 pekee TRA ilivunja rekodi ya makusanyo ya serikali hadi kufikia shilingi trilioni 3.05 ambayo ni sawa na asilimia 103 ya lengo la msingi lililokuwa limewekwa.

Itakumbukwa kuwa Alphayo Kidata wakati anateuliwa kwa mara ya kwanza kushika nafasi hiyo aliikuta TRA imetoka kukusanya kati ya shilingi bilioni 700 hadi 800 kwa mwezi kwa kipindi cha 2016/2017 lakini katika hali ambayo haikutarajiwa kwa muda mfupi tu akiwa ofisini aliiongoza TRA kukusanya kati ya shilingi trilioni 1.2 hadi 1.5 kwa mwezi, takwimu ambazo hazikuwahi kufikiwa na Makamishna wote waliowahi kupita kwenye mamlaka hiyo.

Ikiwa sasa wastani wa TRA kukusanya kodi kwa mwezi unafikia trilioni 2, ndipo tuhuma nzito dhidi yake zinaibuliwa miongoni mwake ni pamoja na ‘mgomo feki’ ulioitishwa na wafanyabishara ambao kiuhasia hadi sasa haijafahamika ni nani aliyeratibu mgomo huo baada ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, uongozi wa soko la kimataifa la Kariakoo Dar es Salaam, Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania (TPSF) na wadau wengine kukana kuutambua mgomo huo.

Jambo TV imekuwa ikipitia mitandao mbalimbali ya kijamii ambapo imeshuhudia baadhi ya wadau/ watumiaji wa mitandao hiyo wengine wakihoji chanzo cha kuibuka kwa tuhuma hizo, lakini pia kuhoji nani aliyepo nyuma ya pazia ya njama hizi zenye nia mbaya dhidi ya mtu ambaye amekuwa akipaisha makusanyo ya mapato ya serikali kila uchwao tena kwa kusimamia sheria na kutocheka na ‘wahuni’?, lakini kubwa kuliko yote haya yanaibuka kwa maslahi ya nani?

Ziko taarifa zisizo rasmi zinazodai kuwa ‘genge’ linaloratibu njama za kumng’oa Kidata TRA ndilo hilohilo lilifanikisha kumng’oa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM (Chama cha Mapinduzi) ambaye kwa sasa ni Mkuu wa mkoa wa Songwe Daniel Chongolo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!