Latest Posts

KIHENZILE: SERIKALI HAITAMVUMILIA MKANDARASI ATAKAYECHELEWESHA MIRADI YA UCHUKUZI

Serikali imesema imedhamiria kuharakisha utekelezaji wa miradi ya uchukuzi katika mkoa wa Kigoma ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara za ndani na za kikanda.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ametoa kauli hiyo baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la abiria katika Bandari ya Kigoma, maendeleo ya Kiwanja cha Ndege cha Kigoma pamoja na soko la Kibirizi.

Amesema Serikali haitamvumilia mtumishi au mkandarasi yeyote atakayesababisha ucheleweshaji wa miradi hiyo, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni ya kimkakati katika kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha usafirishaji katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika.

“Lengo letu ni kuona miradi hii inakamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa ili wananchi waanze kunufaika na huduma bora za usafiri na usafirishaji,” amesema Kihenzile.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigoma, Mganwa Nzota, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi na wadau wengine kuhakikisha hakuna vikwazo vinavyochelewesha utekelezaji wa miradi hiyo.

Naye Meneja wa Bandari ya Kigoma, Edward Mabula, amesema ujenzi wa jengo jipya la abiria umefikia asilimia tisa na unaendelea kulingana na ratiba. Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa bandari kuhudumia abiria wengi zaidi kwa wakati mmoja, na kuimarisha usafiri wa majini ndani na nje ya nchi kupitia Ziwa Tanganyika.

Naibu Waziri huyo yuko mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Wizara ya Uchukuzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!