Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Asasi za Kiraia (NGOs) kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Neema Lugangira, tarehe 5 Agosti 2025, amemkabidhi Mama Justina msaada wa kiti mwendo katika makazi yake yaliyopo Mafumbo, Kata ya Kashai Bukoba Mjini.
Amesema tukio hili ni sehemu ya ishara ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kwa kumuwezesha kumaliza kipindi chake cha uongozi kwa mafanikio makubwa, uadilifu, weledi na kwa hali ya amani.
Lugangira amesema kuwa safari yake ya kiuongozi imekuwa ya kujifunza, kutumikia na kuleta mabadiliko yanayoonekana kwa jamii.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Lugangira amesema “Tulifundwa kwa dhamira, tukapewa jukumu, kazi ikafanyika, na naendelea kusimama katika msingi wa maendeleo yanayoonekana na kugusa maisha ya watu, nikiwa na moyo wa kutumikia Taifa langu kupitia majukwaa mbalimbali.”
Aidha, ameeongeza kuwa anaanza ukurasa mpya wa maisha na kazi, huku akiendelea kuwa na imani thabiti kwa neema ya Mungu, akisisitiza kwa maneno haya “Ukurasa mpya unaanza – na hakika, Mungu ni Mwema.”
Msaada huu ni miongoni mwa hatua zinazodhihirisha dhamira yake ya kuendelea kuwahudumia wananchi, hata baada ya kumaliza muda wake rasmi wa ubunge.