Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne, Agosti 12, 2025, imetupilia mbali maombi ya upande wa utetezi wa Tundu Lissu katika kesi ya marejeo (judicial review) iliyolenga kupinga matumizi ya mashahidi wa siri kama ilivyoombwa na Jamhuri.
Shauri hilo linahusiana na kesi inayomkabili Lissu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo anakabiliwa na tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni. Katika kesi hiyo, Jamhuri iliwasilisha ombi la kuficha baadhi ya mashahidi wakati wakitoa ushahidi wao, hatua iliyopingwa na upande wa utetezi.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Elizabeth Mkwizu. Akizungumza baada ya hukumu, Wakili wa Lissu, Dkt. Rugemeleza Nshala, amesema hawajaridhishwa na uamuzi huo wakidai kuwa unapoka haki ya mshtakiwa kupata utetezi wa haki.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, naye ameeleza kutoridhishwa kwa chama hicho na uamuzi huo, akisema ni kinyume na misingi ya haki. Amebainisha kuwa chama kitakaa na Lissu ili kuangalia uwezekano wa kukata rufaa.
Aidha, Mnyika amewataka wanachama wa CHADEMA kubaki watulivu na kuendelea kujenga chama katika maeneo yao huku taratibu za kisheria zikiendelea kufuatwa.