Mwanaharakati maarufu kwenye mitandao ya kijamii, Mange Kimambi, ambaye anaishi Marekani, amefunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi nchini Tanzania, akidaiwa kujihusisha na utakatishaji wa fedha kiasi cha Sh138.5 milioni.
Kesi hiyo ya jinai namba 000021172 ya mwaka 2025, ilifunguliwa na Jamhuri tangu Agosti 28, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, na imepangwa kutajwa Desemba 4, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, inadaiwa kuwa kati ya Machi 1 na Machi 31, 2022, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Mange alijipatia Sh138.5 milioni akifahamu kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu. Inadaiwa pia alizipata fedha hizo kwa kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kibali pamoja na kuzidai kwa vitisho.
Shtaka hilo linaangukia kifungu 12(1)(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Sura ya 423 ya mwaka 2019, ikisomwa sambamba na Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Asubuhi ya Desemba 2, 2025, video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilimuonesha Mange akithibitisha kuwa amepokea taarifa kuhusu kufunguliwa kwa kesi hiyo, akidai kuwa Serikali ya Tanzania imedhamiria kumrejesha nchini.
Sheria ya kurejeshwa kwa watuhumiwa kutoka nje ya nchi (Extradition Act, 2019) inatambua utakatishaji fedha kama moja ya makosa yanayoweza kupelekea nchi kuomba mtuhumiwa kurejeshwa.
Hatua hiyo mpya inakuja takribani mwezi mmoja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, kueleza kuwa ofisi yake inaangalia uwezekano wa kumchukulia hatua Mange kutokana na tuhuma za kuhamasisha maandamano.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa katika wadhifa huo jijini Dodoma, Johari alisema Serikali inatumia mikataba ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kutathmini uwezekano wa kumrejesha nchini.
“Haiwezekani mtu amekaa nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dada tu hata ukimuangalia muonekano anawaambia watu wakafanye hivi wanaenda kufanya kweli halafu imetokea anaanza kutamba anasema bado nitakuja kivingine, lazima tumkamate. Nakuambia DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka nchini) huyu lazima tumkamate tuangalie kama kuna makubaliano na Marekani, tuangalie tu, tutafikiri tu, lakini hawezi kututambia kwa kiasi hicho yani anakubali kuwa hicho alipanga kukifanya na bado atafanya zaidi sasa tunamuachaje,” alisema AG Johari.
Johari alisema ofisi yake imeanza kufanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, na kwamba hatua zitachukuliwa kwa kuzingatia sheria na mikataba ya kimataifa.
Alisisitiza kuwa matukio ya uharibifu wa mali za umma, ikiwemo kuchomwa kwa gari la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, yamevunja sharia na kwamba Serikali haitaacha jambo hilo bila hatua.