Latest Posts

MAOMBI YA DHARURA YAWASILISHWA MAHAKAMNI, MWANDAMBO ‘AACHIWE AU ASHTAKIWE’

Mawakili wa Mahakama Kuu, Hekima Mwasipu na Philip Mwakilima, wamewasilisha maombi ya dharura ya kisheria (Habeas Corpus) Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya, wakiiomba mahakama iamuru mwanaharakati wa mitandao ya kijamii na mwalimu wa shule ya chekechea, Clemence Kenan Mwandambo, aachiliwe mara moja au afikishwe mahakamani ili kujibu sababu za kuendelea kushikiliwa kwake.

Mwandambo, ambaye hivi karibuni amejijengea umaarufu kupitia ukosoaji wake wa masuala ya kijamii na kauli yake inayosambaa mitandaoni ya “Nachoka mimi mzee wenu Mwandambo”, anadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi tangu Desemba 29, 2025 bila kufunguliwa mashtaka, bila kupewa dhamana na bila kufikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizowasilishwa Januari 9, 2026, mawakili hao wanahoji kuwa kuendelea kumshikilia Mwandambo ni kinyume cha sheria na kunakiuka kwa kiwango kikubwa haki zake za kikatiba, hususan haki ya uhuru wa mtu na haki ya kufikishwa mahakamani ndani ya muda unaotakiwa kisheria. Katika Hati ya Dharura iliyoambatanishwa na maombi hayo, inaelezwa kuwa Mwandambo amezuiliwa kwa muda unaozidi saa 48 zinazoruhusiwa na sheria bila kufikishwa mahakamani.

Mawakili hao pia wanadai kuwa Polisi wamewanyima fursa ya kuonana na mteja wao, pamoja na kuwazuia ndugu na familia yake kumtembelea. Imeelezwa kuwa mke na watoto wa Mwandambo, ambao yeye ndiye mtegemezi wao mkuu, hawajapata nafasi ya kumuona tangu alipokamatwa.

Katika kiapo (affidavit), inaelezwa kuwa Mwandambo alikamatwa kwa mara ya kwanza Novemba 2025 kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo, kisha aliachiliwa kwa dhamana ya Polisi. Hata hivyo, alikamatwa tena Desemba 29, 2025 alipofika Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya kutekeleza masharti ya kuripoti kama ilivyokuwa imeelekezwa.

Upande wa utetezi unaeleza kuwa walipoomba dhamana kwa mara ya pili, maafisa wa Polisi walimtaja Mwandambo kuwa ni “mkaidi” na kudai kuwa alikuwa “mwenye kuelewa kwa shida” maelekezo ya Polisi. Aidha, mawakili hao wanadai kuwa waliambiwa na maafisa wa ndani ya kituo kuwa walikuwa wakitekeleza maagizo ya juu, na kwamba ruhusa kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ilihitajika kwa mtu yeyote kumuona au kumtembelea Mwandambo.

Katika maombi hayo, wadaiwa wametajwa kuwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbeya Mjini, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mbeya Kati na Mkurugenzi wa Mashtaka

Mawakili hao wanaiomba Mahakama Kuu itoe wito wa dharura wa kumfikisha Mwandambo mbele ya jaji na kutoa amri ya kuachiliwa kwake, wakieleza kuwa anaendelea kushikiliwa kinyume cha sheria bila msingi wa kisheria.

Kwa sasa, shauri hilo linasubiri kupangiwa tarehe ya kusikilizwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu jijini Mbeya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!