Latest Posts

MATEMBEZI MSITUNI MAGAMBA YAVUTIA WATALII 300, DC SUMAYE AAHIDI MABORESHO

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Zephaniah Sumaye, ameongoza matembezi ya watalii katika msitu wa hifadhi ya vilima vya Magamba, ambapo zaidi ya watalii 300 wa ndani na nje walishiriki.

Matembezi hayo, yanayojulikana kama Walkathon 2024, yaliandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na yameonesha mafanikio makubwa katika kukuza utalii wa msituni huku yakiungwa mkono na jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhimiza utalii nchini.

Akizungumza wakati wa matembezi hayo, Sumaye alisema: “Matembezi ya utalii msituni ni sehemu ya kutangaza vivutio vya asili na kutengeneza furaha kwa watalii. Tunapojionea vivutio hivi tunahamasika kujenga uchumi wa nchi yetu, huku tukihimarisha afya zetu kupitia mazoezi haya.”

Washiriki wa matembezi waligawanyika katika makundi ya watembea kwa miguu umbali wa kilomita 5, 10, na 20, huku wengine wakifanya safari za baiskeli za kilomita 40. Sumaye alisisitiza kuwa matembezi hayo yanalenga kuimarisha afya za washiriki na kuwafanya watalii kufurahia mandhari ya kipekee ya vilima vya Magamba. “Mimi nafurahi kuona tunahimarisha afya zetu, tunafanya utalii huku tukijenga uchumi wa nchi yetu. Hili ni jambo kubwa sana,” aliongeza.

Mhifadhi Mkuu wa TFS Hifadhi ya Magamba, Christoganus Vyakuta, alisema wilaya ya Lushoto imeendelea kuvutia wageni kutokana na mandhari yake ya asili na hali ya hewa ya baridi.

“Lushoto kuna hali ya hewa ya baridi ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wengi, hasa kutoka nje ya nchi,” alisema Vyakuta. Alibainisha kuwa hadi kufikia Novemba 2024, zaidi ya watalii 5,000 walitembelea vivutio vya hifadhi hiyo, ikiwemo msitu wa Magamba.

Aidha, Sumaye aliahidi maboresho zaidi ya matembezi hayo mwakani ili kuvutia wageni wengi zaidi na kuimarisha ushirikiano wa wananchi katika kukuza utalii wa ndani. “Mwakani tutajitahidi kuongeza maboresho ili kufanya vizuri zaidi ya mwaka huu na kuwa na tamasha kubwa na lipendeze zaidi,” aliahidi.

Matembezi hayo ya msituni, yaliyofanyika kwa mara ya pili, yameonekana kuwa nyenzo muhimu ya kutangaza vivutio vya utalii wa ndani na kusaidia wananchi kuelewa thamani ya hifadhi za misitu katika kukuza uchumi na maisha ya kijamii.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!