Latest Posts

MBEYA DC KUSAJILI SHULE ZA MSINGI ZENYE VIGEZO

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Kutokana na kusambaa kwa taarifa mtandaoni kupitia kipande cha video kikionesha wananchi wa Kitongoji cha Isyesye kijiji cha Igale Kata ya Igale wilayani Mbeya wakilalamikia shule yao shikizi kutosajiliwa licha ya kuwepo kwa miaka 12, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya chini ya Mkurugenzi wake Erica Yegella imefika shuleni hapo ili kutoa ufafanuzi na kuwahakikishia wananchi kuwa shule hiyo itasajiliwa hivi karibuni ikiwa itakidhi vigezo.

Katika kitongoji chao cha Isyesye, kwa muda mrefu wananchi wamekuwa na hoja kuu tatu ambazo ni shule shikizi ya Isyesye kutosajiliwa kwa miaka 12 sasa ili kuwa shule ya msingi, uwepo wa vyumba vitano pekee vya madarasa pamoja na uwepo wa wanafunzi 128.

Akijibu hoja za wananchi hao kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Afisa Elimu wa Wilaya ya Mbeya anayeshughulikia Elimu ya Msingi mwalimu Tanu Kameka, pamoja na maafisa alioambatana nao, amesema jumla ya vyumba vya madarasa viwili vipo na bomba lenye vyumba viwili na ofisi vimejengwa na Serikali na kuhusu idadi ya wanafunzi kuwa 128 ameeleza kuwa takwimu zinaonesha shule hiyo shikizi ina wanafunzi 95.

Afisa Elimu Kameka amewaambia uwepo wa shule hiyo shikizi eneo lao ipo kihalali na ili isajiliwe kuna vigezo vinavyotakiwa hivyo kuwaomba kuendelea kushirikiana ili shule yao pamoja na nyingine kadhaa zisajiliwe rasmi kuwa shule ya msingi ili kuwaondolea adha watoto kutembea umbali mrefu wakiwemo wa kitongoji cha Isyesye wanaosafiri kilomita 5 kwenda shule ya msingi ikizingatiwa shule yao shikizi imefikia darasa la tatu pekee.

Kwa upande wake afisa mthibiti ubora wa shule wilayani Mbeya Bi. Mary Makali, amesema inatakiwa iwe na vyumba vya madarasa 6, ofisi za walimu 2, matundu ya vyoo vya wanafunzi wakike 6, wavulana matundu 5 na vyoo vya walimu Matundu 2.

“Shule shikizi zimewekwa na Serikali kwa utaratibu lakini shule hizi zinaweza kuwa shule kamili endapo wanakijiji wataweza kuongeza madarasa na kukidhi vigezo vyote vya kuwa shule kamili”, ameeleza Makali.

Wananchi hao wameahidi kuwekeza nguvu kwenye shule hiyo ili na shule ya Isyesye iingie kwenye idadi ya shule zitakazosajiliwa mwaka huu 2025 ili kuzuia watoto kwenda umbali wa kilomita 5 kufuata shule mama ya msingi Igale ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imetenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza shule shikizi zenye sifa ya kuwa shule kamili.

Katika hayo yote wananchi wanahimizwa kuendelea kujitoa kwenye shughuli za maendeleo na pia kushirikiana na Serikali kuhakikisha shule hiyo inasajiliwa baada ya kutimiza vigezo ikizingatiwa wilaya ya Mbeya ina shule shikizi 29 na tayari shule 9 zilisajiliwa kwa kipindi cha mwaka 2022.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!