Latest Posts

MBUNGE MULUGO ASISITIZA NIDHAMU KWA WANAFUNZI SIRI YA UFAULU

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mbeya Patrick Mwalunenge amewatunuku vyeti wanafunzi 112 wa shule ya sekondari St. Marcus iliyopo Iwambi jijini Mbeya na kuwataka wanafunzi kutunza nidhamu ili kufanikiwa maishani mwao.

Mwenyekiti Mwalunenge amesema hayo wakati akizungumza kwenye mahafali ya tisa ya kuwaaga wahitimu 112 wa kidato cha nne katika shule hiyo.

Mwalunenge ameipongeza shule ya St. Marcus kwa kuwa miongoni mwa shule bora kumi katika kanda ya nyanda za juu kusini na shule ya nne kwa ubora katika mkoa wa Mbeya na kusisitiza nidhamu kuendelea kusimamiwa ipasavyo kwa wanafunzi kuelekea masomo ya elimu ya juu.

Hata hivyo ameishauri shule hiyo kuanzisha mafunzo ya kilimo kutokana na ukweli kwamba ajira Serikali ni chache na kilimo kimeajiri watu wengi ndani na nje ya nchi wazo ambalo limepokelewa na mkurugenzi wa shule hiyo mwalimu Philip Mulugo.

Akizungumza kwenye mahafali hayo, mkurugenzi wa shule za awali, msingi na sekondari St. Marcus Mwal. Phillip Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Songwe Mkoani Songwe, amesema shule yake inafanya vizuri katika nyanja mbalimbali hasa kitaaluma kutokana na kusimamia nidhamu, ubora na juhudi katika ujifunzaji na ufundishaji.

Mulugo amesema katika kuhakikisha shule inaendelea kufanya vizuri wamekuwa wakiwaadhibu watoto kwa mujibu wa mwongozo wa Serikali wale wanaokaidi na kutokuwa na nidhamu.

“Ndugu mgeni rasmi (Patrick Mwalunenge), St. Marcus tunachapa fimbo, mimi huwa simung’unyi maneno, hata nilivyokuwa Naibu Waziri wa Elimu nilikuwa ninawambia walimu chapeni fimbo ilimradi kwa kuzingatia mwongozo, tuna mwongozo kuchapa fimbo nne na anayechapa ni mkuu wa shule, kwahiyo sisi tunachapa fimbo na ndio maana mnaona watoto hawa (wahitimu) wana nidhamu na wameiva kwelikweli (kitaaluma)”, amesema Mkurugenzi wa shule za St. Marcus Philip Mulugo.

Hata hivyo watoto hao kupitia risala yao wameeleza kujiandaa ipasavyo kuukabili mtihani wao wa mwisho baadaye mwezi ujao kwa kuhakikisha wanapata ufaulu wa daraja A ambapo jumla ya wanafunzi 112 (wakike 54 na wakiume 58) wanatarajia kuungana na wenzao kote nchini kufanya mitihani yao ya mwisho kuanzia Novemba 11, 2024.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!