Na Josea Sinkala, Mbeya.
Wataalam wa sheria kutoka kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, wameendelea na ziara yao katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya na kukutana na wananchi mbalimbali kwa ajili ya utoaji elimu na ushauri wa masuala ya kisheria na kesi mbalimbali hasa za kisheria.
Ziara hiyo imeendelea ikiwemo katika maeneo ya Mlima Njiwa, Matundasi na Chunya Mjini kwa wataalamu hao kukutana na makundi mbalimbali ya wananchi kutoa elimu na ushauri wa masuala ya kisheria na migogoro ya ardhi.
Wakili Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ambaye ni Mratibu wa Mama Samia Legal Aid Campaign mkoa wa Mbeya Emmanuel Mbega na wakili Aveline Ombock, wamefika katika kata ya Matundasi kwa ajili ya kutatua mgogoro mmoja wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka sita ambapo familia moja ya Abeli Benzi ambaye aliingia kwenye mgogoro na mfanyabiashara na mwekezaji Fedilis Ntanyinya baada ya kumuuzia eneo lake kienyeji bila kuandikishana mwaka 2018 lakini baadaye makubaliano yao ya mwekezaji huyo kumjengea nyumba nyingine ili amuachie ardhi ya awali hayakufanikiwa kama ilivyopangwa.
Familia hiyo ilimuuzia mfanyabiashara na mwekezaji Fidel Ntanyinya eneo lao lililopo kando ya barabara kuu ya Chunya Makongolosi kwa gharama ya shilingi 1,400,000/= (Shilingi milioni moja na lakini nne) kwa makubaliano pia ya kumjengea nyumba eneo lingine la familia jambo walilodai Fidel Ntanyinya hakulitekeleza kwa wakati hali iliyowalazimu kwenda Baraza la Kata na Mahakamani bila mafanikio.
Kwa upande wake Fidel Ntanyinya ambaye ni mfanyabiashara mkoani Mbeya, ameishukuru timu ya wataalam wa sheria kupitia Samia Legal Aid kwa kuwafikia wananchi katika maeneo yao kuhakikisha wanawashauri ili kumaliza tofauti zao akiwemo yeye mwenyewe akisema mawakili hao wamekuwa weledi hata kufanikiwa kumaliza mgogoro huo kwa muda mfupi kwani yeye kama mfanyabiashara na mwekezaji mgogoro huo ulikuwa ukimuathiri kiuchumi zaidi akiiomba timu hiyo kufika zaidi vijijini hasa kwenye ngazi za kata akidai kuna migogoro mingi.
Baada ya kusikiliza pande zote timu ya kisheria ya Samia Legal Aid ilizitaka pande hizo mbili kuketi meza moja kwa mazungumzo makubaliano ambapo familia ya Abel Benzi na mkewe imetaka kulipwa shilingi milioni mbili (Tshs 2,000,000/=) ili iweze kuachia eneo hilo jambo ambalo limetekelezwa na Fidel Ntanyinya na kulipa fedha hizo mbele ya timu ya Mama Samia.
Naye Diwani wa Kata ya Matundasi wilayani Chunya Kimo Choga, pamoja na kushukuru mgogoro huo kumalizika katika eneo lake pia ameeleza kuwa amani imerejea kwenye kata yake kupitia mgogoro uliokuwepo baina ya wawili hao tangu mwaka 2018.
Diwani wa Kata ya Makongolosi Kassim Haule, amesema kwa kipindi kifupi timu hiyo katika Kata ya Makongolosi imesikiliza migogoro mingi hususani ya ardhi, ndoa na mirathi na kuomba msaada wa kisheria uwe endelevu Ili kuwasaidia wananchi wengine hususani wasio na uwezo wa kwenda mahakamani na kumudu gharama za mawakili.
Timu ya mawakili kutoka kwenye kampeni ya ‘Samia Legal Aid’ inatarajiwa kutamatika Machi 10, 2025 ambapo wananchi kupitia mawakili hao wanafikiwa bure na kushauriwa mambo mbalimbali yahusuyo sheria na masuala ya migogoro ya ardhi, mirathi na ndoa ili kuhakikisha jamii inaishi kwa amani na utulivu na kuchochea maendeleo ya Taifa