Chama cha Ushirika cha Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Dhahabu cha Mgusu, chenye makao yake mkoani Geita, kimekabidhiwa tuzo ya heshima kwa kuwa miongoni mwa vyama vinavyofanya vizuri nchini kupitia sekta ya madini.
Tuzo hiyo imetolewa na Waziri Mkuu katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Vyama vya Ushirika yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Akikabidhi tuzo hiyo kwa Mwenyekiti wa Ushirika huo, Masabile Modesti, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Geita, Doreen Mwanri, amesema chama hicho kimepata heshima hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika kuongeza mapato ya serikali na kuwa miongoni mwa vyama vyenye uongozi imara.
Sambamba na tuzo hiyo, Mwanri amekabidhi pia cheti cha pongezi kinachotambua mchango wa chama hicho katika kuendeleza ushirika.
Baada ya kupokea tuzo na vyeti hivyo, Mwenyekiti Masabile Modesti ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwatia moyo kupitia zawadi na hati za kutambua mafanikio yao, akisema hatua hiyo imeongeza nguvu na thamani katika shughuli zao.
Kwa upande wake, Katibu wa Ushirika huo, Zacharia Nshoma, amesema wanachama wote wanayo sababu ya kujipongeza kwani wamekuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha chama kinapata mafanikio hayo.