Mbunge wa Jimbo la Msalala lililopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Iddi Kassim Iddi amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Khamis Katimba kutembelea na kukagua miradi ya kimkakati iliyopo kwenye halmashauri hiyo na kuchukua hatua za kuhakikisha inakamilika katika ubora ambao umepangwa na serikali.
Mbunge Iddi ametoa kauli hiyo kutokana na malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Kabondo Kata ya Mwanase, ambao wamedai pamoja na kila kaya kuchangia kiasi cha Shilingi elfu 40 na serikali kuu kutoa zaidi ya Shilingi milioni 50, mradi wa ujenzi wa zahanati umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu na kushindwa kukamilika, hali ambayo imepelekea kwa sasa jengo lake kuanza kubomoka kutokana na kushindwa kuendelezwa.
“Mbunge nataka kujua sisi wananchi tumechangishwa kila kaya elfu 40 lakini, hii Zahanati wajumbe wanaoteuliwa kusimamia ni wakina nani? Ujenzi huu haujawahi kukamilika, tangu umeanza una miaka miwili ninavyokumbuka, sasa nina mashaka kuna dalili za upigaji haiwezekani mradi mkubwa kama huu kuchukua miaka yote hiyo bila kukamilika na cha kushangaza ukifika pale tayari jengo limeanza kuwa na nyufa kubwa” Alisema Salum Masasila Changalawe.
Kufuatia madai hayo mbunge Iddi akamtaka msimamizi wa mradi huo ambaye ni mganga mfawidhi Zahanati ya Mwanase Don Leornad, kutoa ufafanuzi wa suala hilo ambapo amesema fedha zote ziliingia kupitia akaunti ya zahanati ya Mwanase, million 50 na awamu ya pili milioni 10 ambapo waliona busara kushirikisha wajumbe wa Mwanase na wa kijiji cha Kabondo.
“Ni kweli kuna mipasuko imetokea lakini wataalamu walifika wakasema mzigo ambao wameupata kwa sasa kutokana na kusimama kwa muda mrefu jengo limeanza kushuka upya, lakini hata makisio ya kutekeleza mradi wa Zahanati ya Kabondo haijakisiwa kwani kawaida ilitakiwa iwe zaidi ya milioni 80 bado hazijafikiwa” Ameeleza Don Leornad.
Hata hivyo Mbunge Iddi ameonesha kutokuridhishwa na majibu ya msimamizi wa mradi huo kutokana na kuchukua muda na kuonesha kuwa umetekelezwa bila ya kufuatiliwa na kiongozi yeyote wa Halmashauri.
“Nimuombe mkurugenzi miradi hii serikali inatoa fedha nyingi sana, sioni sababu ya yeye kushindwa kufuatilia na kufanya ukaguzi kwenye hii miradi nimuombe aje afuatilie, kwenye jimbo zima tulikuwa na zahanati 34 hazijakamilika, na hapa nilileta milioni 50. Naomba niwahakikishie wananchi wangu, mimi mbunge wenu mmeniamini mkanichagua niwatumikie na kuwakilisha kero zenu, niwahakikishie sitakuwa chanzo au sababu ya kuwakwamisha kufikia ndoto za maendeleo ambazo mnazihitaji, nitashughulika na yeyote ambaye atacheza na mali ya umma” Alisema Iddi Kassim.
Mbunge Iddi amekamilisha ziara yake kwenye Kata ya Mwanase kwa kusilikiliza kero za wananchi pamoja na kuzitolea ufumbuzi kwenye vijiji vya Kabondo, Mwamandi, Nata na Mwakuhenga.