Shauri namba 8323/2025 lililofunguliwa na Saidi Issa Mzee na wenzake dhidi ya bodi ya wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo limeahirishwa mpaka Julai 28, 2025.
Leo shauri hilo lilikuwa mbele ya Jaji Hamidu Mwanga ambapo hoja za kisheria pande mbili za walalamikaji na walalamikiwa pamoja na maelezo ya kumkataa jaji kutoka upande wa walalamikiwa yaliwasilishwa na kusomwa mahakamani hapo na Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika.
Mnyika aliieleza mahakama sababu kuu ya wao kumkataa Jaji Mwanga, ikiwa ni wao kunyimwa fursa ya kupata uwakilishi mahakamani siku ya Juni 10, baada ya wakili Jebra Kambole kujiondoa kwenye kesi hiyo.
Mnyika ameileza mahakama kuwa baada ya Jebra kujiondoa kwenye kesi alimuomba Jaji awaarifu wateja wake (bodi ya wadhamini wa CHADEMA) ili waweze kupata uwakilishi wa wakili mwingine au wajiwakilishe lakini jaji hakutoa nafasi aliendelea na kesi mpaka alipotoa maamuzi.

Sababu nyingine ya kumkataa Jaji Mwanga ni Wakili Jebra aliomba ahirisho la kesi ili kwenda kushiriki mazishi ya ndugu wawili wa Wakili Hekima Mwasipu ambae Wakili mwenzake kwenye kesi hiyo lakini Jaji alikataa.
Hoja nyingine ni kwamba Mei 21, 2025Â Maulida Anna Komu aliwasilisha mahakamani notisi ya kujitoa kwenye kesi na Mei 30, 2025 ambapo Wakili Dkt. Nshala alimuandikia Jaji Barua ya kumuomba kuwaita mawakili wa pande zote kujadili barua hiyo na athari za kujitoa kwa mama Komu na Jaji hakufanya hivyo.
Hata hivyo Juni 10, shauri lilipoitwa mawakili wa upande wa walalamikaji waliieleza mahakama kuwa Mama Komu yupo mahakamani na Jaji akaelekeza walalamikaji kueleza juu ya kujitoa kwa Mama komu na sio athari za kujitoa kwake.
Mnyika amesema Jaji Mwanga hakumpa nafasi Wakili Edson Kilatu ambaye ndiye alifaili kiapo cha kujitoa kwa Mama Komu badala yake alitoa maagizo ya wakili kilatu kuchunguzwa na polisi. Hivyo upande wa walalamikiwa haukupata kusikilizwa wala Wakili hakupata nafasi ya kujieleza mbele ya mahakama.
Sababu zingine ni pamoja na agizo lililotoka la kutaka bodi ya wadhamini kutotumia mali za CHADEMA pamoja na Katibu kuwa agizo hilo linaathiri mali za chama na kusababisha kuibiwa na hata kupotea.
Baada ya Mnyika kuwasilisha hoja zake mawakili wa utetezi walipata nafasi ya kujenga hoja za kisheria kumtetea Mnyika na baadae upande wa walalamikaji walijibu hoja na mwisho Jaji Hamidu Mwanga alisema anataka muda wiki mbili kuandaa uamuzi na Julai 28 atatoa uamuzi wa kuendelea na kesi au lah.