Wafanyabiashara zaidi ya 500 wamepata hasara kubwa baada ya Soko la Mashine Tatu lililopo katika Manispaa ya Iringa kuteketea kwa moto mkubwa usiku wa kuamkia leo.
Moto huo uliotokea ghafla usiku uliunguza vibanda vya biashara na mali mbalimbali huku wakazi na wafanyabiashara wakiishia kushuhudia juhudi zao zikiteketea pasipo kuweza kuokoa mali zao kutokana na kasi ya moto.
“Tumehangaika kujenga biashara hizi kwa muda mrefu, leo zimeteketea mbele ya macho yetu. Hakuna tulichookoa,” amesema Mariamu Ubamba, mmoja wa wafanyabiashara waliopoteza kila kitu kwenye soko hilo.
Hamis Kiyemba, mfanyabiashara mwingine ameeleza kwa uchungu: “Nimeteketezewa kila kitu. Sina hata mtaji wa kuanzia. Tunaomba msaada kutoka serikalini na kwa wadau wengine ili kurejea katika maisha ya kawaida.”
Kwa upande wake, Marry Ilomo ameongeza: “Ni huzuni tupu. Tunahitaji msaada wa haraka ili kujikimu. Hakuna aliyepona.”
Mwenyekiti wa Masoko wa Manispaa ya Iringa, Rafael Ngulo amesema tukio hilo limeathiri familia nyingi na limepunguza kasi ya mzunguko wa uchumi katika eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, ametembelea eneo la tukio na kueleza kuwa bado chanzo cha moto hakijafahamika, lakini vyombo husika vimeagizwa kufanya uchunguzi mara moja.
Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Iringa, Jackline Mtei, amesema kuwa walipokea taarifa kwa haraka na kufika eneo la tukio kwa muda, wakifanikiwa kuzuia moto usienee zaidi.
“Moto ulikuwa mkubwa sana. Tumefanikiwa kuuzima kwa kushirikiana na wananchi, lakini uharibifu tayari ulikuwa mkubwa.”
Mpaka sasa, mamlaka za serikali na manispaa zinaendelea na tathmini ya uharibifu ili kujua kiasi halisi cha hasara, huku wito ukitolewa kwa wamiliki wa biashara kuwekeza katika vifaa vya tahadhari ya moto.