Mradi wa umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Nyakanazi, mkoani Kagera hadi Kidahwe, mkoani Kigoma, umefikia asilimia 99 ya utekelezaji, huku umeme huo ukiwa umeanza kutumika rasmi tangu Desemba 12, 2024.
Mradi huu, unaogharimu shilingi bilioni 5, unatajwa kuongeza uwezo wa matumizi ya umeme kutoka megawati 16.5 hadi 24, huku pia ukipunguza gharama kubwa iliyokuwa ikitumika kuendesha mitambo ya zamani iliyotegemea mafuta kuzalisha nishati hiyo.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Jamal Tamim, amesema kuwa mradi huo unafungua fursa mpya kwa wawekezaji katika sekta ya viwanda mkoani Kigoma.
“Awali, wawekezaji wengi waliokuwa na nia ya kuwekeza katika viwanda walishindwa kutokana na ukosefu wa umeme wa uhakika na wa kutosha. Sasa, kwa kukamilika kwa mradi huu, mazingira ya uwekezaji yameboreshwa zaidi,” amesema Tamim.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Abuya, amesema kuwa mradi huu unatimia kwa wakati muafaka, ukihamasisha utekelezaji wa dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuufanya Mkoa wa Kigoma kuwa kitovu cha biashara na uchumi kwa ukanda wa Magharibi.
“Kigoma inapakana na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia kupitia Ziwa Tanganyika. Uwepo wa viwanda utafungua milango kwa wafanyabiashara wa nchi hizi kuja Kigoma badala ya kwenda maeneo mengine, jambo litakalosaidia kuinua uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla,” amesema Abuya.
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Deogratius Nsokolo, ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huu ni hatua muhimu kwa wakazi wa Kigoma, kwani umeme wa uhakika utahamasisha uwekezaji na kuongeza fursa za ajira.
Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Karim Namahala, amesema kuwa mradi huo unahusisha ujenzi wa njia tano za usambazaji wa umeme wa msongo wa kilovoti 33 kutoka kituo cha kupoza umeme cha Kidahwe kuelekea wilaya za Buhigwe, Kigoma Mjini, Kasulu, Uvinza na Ilagala. Hii itaongeza usambazaji wa nishati hiyo na kuhakikisha mikoa hiyo inapata umeme wa kutosha kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kwa kukamilika kwa mradi huu, Kigoma inajiweka katika nafasi bora zaidi ya kuvutia wawekezaji na kuongeza kasi ya maendeleo, huku wananchi wakianza kuona manufaa ya uwekezaji huu mkubwa wa serikali.