Mtandao wa Wanawake na Watetezi wa Haki za Binadamu umetoa wito mzito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kutoa tamko rasmi la kulaani kile walichokiita vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ukandamizaji wa demokrasia, na unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa dhidi ya wananchi, hususan wanawake, kufuatia kukamatwa kwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Mtandao huo umesema kupitia taarifa yao ya siku ya Jumanne Aprili 29, 2025 kuwa ukimya wa Rais Samia hadi sasa unaacha maswali mengi kwa umma na unaweza kutafsiriwa kama kuruhusu au kufumbia macho dhuluma dhidi ya raia wake, kinyume cha maadili ya haki, utu na usawa aliyoahidi kuyasimamia.
“Taarifa mbalimbali zimeonesha wanawake wakidhalilishwa, kuvuliwa nguo na kuteswa bila sababu, hali inayoashiria matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wasio na silaha. Vitendo hivi vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977”, imeeleza sehemu ya taarifa yao.
Wanaharakati hao wameelezea kusikitishwa kwao na taarifa za wananchi, wakiwemo wanawake, waliokwenda kufuatilia kesi ya Tundu Lissu, kukamatwa kinyume cha sheria, kupigwa, kutishiwa maisha na wengine kudhalilishwa kwa kuvuliwa nguo hadharani, hali ambayo wamesema ni ukiukwaji mkubwa wa utu wa binadamu.
Kwa mujibu wa mtandao huo, matendo hayo yanayodaiwa kufanywa na vyombo vya dola yanakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, hususan Ibara ya 12 na 13 (Usawa mbele ya sheria na heshima ya utu wa binadamu), Ibara ya 15 (Uhuru wa mtu binafsi), Ibara ya 18 (Uhuru wa maoni na kupata taarifa), Ibara ya 20 (Haki ya mikusanyiko ya amani) na Ibara ya 107A na 107B (Uhuru wa mahakama na haki ya usikilizwaji wa haki)
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, Jumatatu, Aprili 28, 2025, alikanusha madai kuwa Jeshi la Polisi liliwapiga au kuwatesa wanachama wa CHADEMA waliokamatwa hivi karibuni, akibainisha kuwa walikamatwa viongozi wawili pekee wa chama hicho, ambao ni Makamu Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu John Mnyika.
Akizungumza na chombo cha habari cha Jamii Forums, Muliro alisema, “Sisi tuliwakamata Heche na Mnyika, waliuzeni kama wana majeraha. Hao wengine tuwakamate tuwapeleke wapi? Waulizeni walikamatwa wapi?” alihoji, akisisitiza kuwa si kila aliyepata majeraha siku hiyo alijeruhiwa na Polisi.
Katika hatua nyingine, wanaharakati hao wamelalamikia uamuzi wa Mahakama kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya mtandao (virtual hearing) bila kumleta mtuhumiwa mahakamani, wakieleza kuwa hali hiyo inahatarisha dhana ya uwazi katika mchakato wa haki na kuondoa nafasi ya wananchi kushiriki katika mifumo ya utoaji wa haki kwa njia ya wazi.
Pamoja na mambo mengine, katika wito wao kwa vyombo vya dola na mihimili ya kikatiba, wanaharakati wametaka kuachiliwa huru kwa wote waliokamatwa kinyume cha sheria, uchunguzi huru na wa haraka kufanyika kuhusu matumizi ya nguvu na manyanyaso kwa raia, kuwajibishwa kwa wote waliohusika na mateso, manyanyaso au vifo, kulindwa kwa uhuru wa mahakama dhidi ya ushawishi wa mihimili mingine
Mtandao huo pia umetoa wito kwa jamii ya kimataifa, mashirika ya haki za binadamu na vyombo vya habari kuendelea kufuatilia na kushikamana na Watanzania katika mapambano ya kutetea utu, usawa na uhuru wa kikatiba.