Wito umetolewa kwa wenye madai mbalimbali ya haki kufuata sheria na taratibu zilizopo katika kudai haki zao badala ya kushinikiza kusikilizwa kupitia njia zenye kuvunja amani ya nchi pamoja na kuharibu mali za umma na za watu binafsi wasiokuwa na hatia.
Ushauri huo umetolewa wakati huu ambao bado watanzania wanakumbuka na kueleza madhila waliyoyapitia kufuatia vurugu na uharibifu wa Siku na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, suala ambalo limepelekea watu wengi kueleza athari za kiuchumi kutokana na wizi, uchomaji moto na uharibifu wa mali hasa Vituo vya mafuta, maduka na katika sehemu za starehe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mzee Said Ally Mwegelo amesisitiza kufuata njia sahihi katika madai ya haki, akisema haki kamwe haiwezi kupatikana katika sehemu isiyokuwa na amani na utulivu kama ilivyoshuhudiwa mwishoni mwa mwezi uliopita.
Ameeleza kusikitishwa pia na uharibifu mkubwa wa mali za watu wasiokuwa na hatia na wasiojihusisha na siasa, akiwataka wale wote wenye tabia na mwamko wa kujihusisha na uharibifu kuacha mara moja na badala yake wafuate sheria na miongozo iliyopo nchini ili kulinda amani na utulivu.