NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mbeya Christopher Uhagile, amesema Chama hicho kina nguvu, ujasiri na uwezo mkubwa wa kushinda uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji kutokana na uimara wake katika kuwatumikia wananchi.
Uhagile amesema hayo Novemba 07, 2024 wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM kata ya Itezi Uyole jijini Mbeya walipokutana kwa ajili ya mwendelezo wa vikao vyao kuelekea uchaguzi huo, kikao kilichoambatana na kumpokea aliyekuwa katibu wa Baraza la wanawake wa CHADEMA kata ya Itezi Sophia Mwakomo.
Katibu huyo wa itikadi na uenezi mkoani Mbeya, amesema kazi zinazoendelea kufanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaonekana na ndio zinaendelea kuwavuta viongozi na wanachama wa upinzani hasa CHADEMA kukirudia chama hicho kikongwe barani Afrika.
“Yaani uchaguzi huu (Serikali za mitaa) kuna watu wanakwenda kupigwa kipigo huko, moto unawaka, hizi zote ni salamu za tarehe 27, 2024 kwahiyo hapa tunatuma salamu hapa Itezi, jiji la Mbeya na mkoa mzima wa Mbeya kwamba CCM inakwenda kushinda kwa kishindo kwa sababu ya kazi anazofanya mwenyekiti wa Chama chetu na Rais wa nchi yetu (Dkt. Samia Suluhu Hassan) pamoja na Dkt. Tulia Ackson (Mbunge wa Mbeya mjini)”, amesema Christopher Uhagile, katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Mbeya.
Pamoja na hayo ameendelea kuwakaribisha wananchi wengine wasio wanachama wa CCM kujiunga na Chama hicho.
Sophia Mwakomo ambaye alikuwa Katibu wa BAWACHA kata ya Itezi anasema ameshawishika na utendaji kazi wa viongozi wa CCM wakiongozwa na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Mbeya mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson huku akihusisha na kunyimwa nafasi ya kugombea nafasi ndani ya Chama chake cha zamani (CHADEMA) kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu akidaiwa kuwa hafanyi kazi za Chama jambo alilolipinga vikali.
Mwenyekiti wa CCM kata ya Itezi Gervas Lonje, amesema huo ni mwendelezo wa kuendelea kuwapokea viongozi na wanachama mbalimbali kutoka upinzani kwani hivi karibuni aliyekuwa Katibu mwenezi wa CHADEMA kata hiyo (Itezi) Leonorah Maneno alikihama Chama hicho na kujiunga na CCM huku katibu mwenezi wa kata hiyo Raphael Mwaitege akisema huo ni usajili wa dirisha dogo na kuanzia Januari 2025 litafunguliwa dirisha kubwa kwa ajili ya kuwapokea viongozi na wanachama mbalimbali kutoka vyama vya upinzani.