Latest Posts

MWENYEKITI UWT NJOMBE ARUDISHA TABASAMU KWA KIJANA MWENYE ULEMAVU WA MIGUU

News, Njombe.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe, Dkt. Scholastika Kevela, ametumia sikukuu ya Mwaka Mpya kumfariji Amir Mtendwa, kijana mwenye ulemavu wa kupooza miguu, kwa kumkabidhi zawadi ya kiti mwendo.

Amir, mkazi wa Kata ya Uhenga wilayani Wanging’ombe, alipooza miguu akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu kutokana na homa kali aliyoipata wakati akijifunza kusimama. Tangu wakati huo, kijana huyo amekuwa akikabiliwa na changamoto kubwa za ulemavu.

Dkt. Scholastika, akizungumza Januari 2, 2025, wakati wa kumkabidhi zawadi hiyo, alisema kiti mwendo hicho kinalenga kumrahisishia kijana huyo kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kuboresha maisha yake.

“Tumeona ni muhimu kumfariji mwenzetu kutoka Uhenga kwa kumpatia kiti mwendo kama zawadi ya Mwaka Mpya. Tunatoa hii sadaka kwa sababu tumejaaliwa kila kitu, lakini mwenzetu amepungukiwa. Tunaamini msaada huu utakuwa wa manufaa makubwa kwake,” amesema Dkt. Scholastika.

Shangazi wa Amir ameeleza furaha yake kwa msaada huo, akibainisha kuwa homa iliyompata kijana huyo iliwaletea changamoto kubwa kama familia, lakini sasa kiti mwendo kitamrahisishia maisha. “Tunaishukuru sana familia ya Dkt. Scholastika kwa msaada huu wa kipekee kwa kijana wetu,” amesema shangazi huyo.

Aidha, Dkt. Scholastika ametoa wito kwa wadau na wananchi wa Mkoa wa Njombe kuwasaidia watu wenye uhitaji, akisisitiza kuwa sadaka ya aina hiyo ni yenye thamani kubwa na yenye kudumu hata baada ya maisha haya.

“Watu wenye uhitaji wapo wengi, na ni jukumu letu kuhakikisha tunawafariji na kurudisha tabasamu usoni mwao. Hii ni moja ya njia bora ya kuonesha ubinadamu na upendo wa kweli,” ameongeza Dkt. Scholastika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!