Wito umetolewa kwa Vijana kujiepusha na makundi yasiyofaa pamoja na kutofuata kila wanachoambiwa kwenye Mitandao ya Kijamii nchini katika kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuwepo.
Wito huo umetolewa na Mzee Ally Bomba Omar, Mkazi wa Tandika Mabatini Mkoani Dar Es Salaam, akieleza kuwa tangu kuzaliwa kwake Mwaka 1949 hakuwa kushuhudia vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
“Tangu kipindi cha Mwalimu Nyerere tulikuwa tunaishi kwa amani, matatizo haya yaliyotokea hapa yamenishangaza na watu hawa sijui wametokea wapi. Sisi tusiokuwa nacho na tuliozoea kununua unga nusu kilo nusu kilo tuliteseka sana na bahati mbaya hata ukiwa na visenti unanunua wapi vitu? Maduka yote yalikuwa yamefungwa.” Amesema Mzee Bomba.
Mzee huyo amefahamisha kuwa ana amini kwamba kila mmoja ana akili timamu, akisema makundi mabaya yatawapoteza, akisema maandamano yasiyo rasmi yanaleta matatizo mengi ikiwemo vifo, majeraha na uharibifu wa mali na maisha.