Latest Posts

PAC YAFICHUA KASORO KATIKA MRADI WA UWANJA WA NDEGE WA MSALATO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imebaini kasoro kadhaa katika utekelezaji wa Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, jijini Dodoma, zikiwemo ajira kwa wahandisi wasiosajiliwa, ujenzi bila vibali, ongezeko la gharama, na ucheleweshaji wa malipo.

Mwenyekiti wa PAC, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka, akiwasilisha ripoti ya kamati kwa mwaka 2024 Februari 12, 2025, amesema ukaguzi wao umebaini uwepo wa wahandisi wasiosajiliwa waliotekeleza mradi huo kinyume na Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Usajili wa Wahandisi ya mwaka 2007.

Aidha, ripoti hiyo pia imebaini kuanza kwa ujenzi wa majengo bila hati miliki wala vibali vya ujenzi, jambo lililokiuka Kanuni Na. 4(1) ya Kanuni za Ujenzi wa Mipango Miji ya mwaka 2018, ambayo inataka ujenzi wowote kupata kibali kutoka mamlaka husika.

PAC pia imeeleza kuwa dosari katika upembuzi yakinifu zilisababisha ongezeko la gharama ya mradi kwa Shilingi Bilioni 3.04. Sababu kuu ya dosari hiyo ilikuwa matumizi ya ndege nyuki (drones) katika kupima eneo bila kusafisha vichaka, hali iliyopelekea tafsiri isiyo sahihi ya usawa wa ardhi.

Ripoti hiyo imebaini pia malipo ya Shilingi Bilioni 5.729 kwa kazi zisizoidhinishwa na Bodi ya Zabuni na malipo ya riba ya Shilingi Milioni 303.814 kutokana na ucheleweshaji wa malipo kwa mkandarasi kwa kati ya siku 8 hadi 70.

PAC imeitaka serikali kuhakikisha kuwa miradi ya kimkakati inatekelezwa kwa kuzingatia sheria na taratibu ili kuepusha upotevu wa fedha za umma.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!