Wakazi wa kijiji cha Maranje kata ya Mtiniko Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara wameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi mkubwa wa kiwanda cha korosho katika maeneo yao kitakachowawezesha kupata ajira.
Hayo yameelezwa wakati wa utiaji saini ujenzi wa kongani la viwanda kati ya mkandarasi wa kampuni ya Malagarasi Enterprises and Contractor Limited na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) unaotekelezwa katika kijiji hicho.
Mkazi wa Kijiji cha Maranje Dadi Salumu amesema uwepo wa mradi huo ni fursa kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo na jirani kwa sababu wana imani kuwa watapata ajira kupitia kazi mbalimbali kiwandani hapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Maranje, Issa Hassan amesema kupitia ujenzi huo ni fursa kubwa kwa vijana kuona namna ya kutoka walipo kwa sasa na kusonga mbele kimaendeleo hivyo ni vema kwa wale watakaokuwa sehemu ya ajira hizo kufanya kazi na kuwa waaminifu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya CBT, Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesema bodi hiyo inatekeleza kongani la viwanda kijijini hapo ikiwa ni agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Septemba 2023 alipofanya ziara ya kikazi katika mikoa ya Mtwara na Lindi lakini pia kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayowataka kuzalisha tani milioni 1 ifikapo mwaka 2030.
‘’Mradi huu unaenda kutimiza malengo na kufanya wakulima waweze kupata tija kwa zao hili, kusainiwa kwa mkataba huu ni mwanzo wa bodi kumiliki viwanda vya pamoja ya kubangua korosho na kusindika bidhaa zake.’’Amesema Mwanjile.Â
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amemtaka mwekezaji katika mradi huo kuwapa kipaumbele wakazi wa kijiji hicho, maeneo jirani pamoja na Wanamtwara kwa ujumla ili waweze kupata ajira na fursa mbalimbali zinazotokana na mradi huo.
Aidha ameiagiza Bodi ya CBT na Mkandarasi wa kampuni hiyo kuzingatia matakwa ya mkataba uliosainiwa kwa ajili ya ujenzi wa ghala mbili zitakazogharimu Shilingi bilioni 2.797 ambapo pia kutakuwa na ujenzi wa majengo mbalimbali ikiwamo ya viwanda.