Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, amesisitiza umuhimu wa kulinda ubora na usalama wa korosho za wakulima, akielekeza viongozi wa vyama vya ushirika kuhakikisha mazao yanahifadhiwa kwa usahihi na kulipwa kwa wakati ili kuzuia hasara kwa wakulima.
Katika ziara yake Desemba 4, 2025 kwenye ghala la Mtimbwilimbi katika Halmashauri ya Mji Nanyamba, Kanali Sawala amesema uangalizi hafifu katika uhifadhi wa korosho unaweza kusababisha upotevu wa mazao na kupunguza mapato ya wakulima, hasa wakati msimu wa mvua unakaribia.

Amesema viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu wanapaswa kutekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kuzingatia mwongozo wa usalama wa mazao na utabiri wa hali ya hewa, ili kuhakikisha korosho zinabaki katika ubora unaohitajika na soko.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa vyama vya ushirika kutochelewesha malipo kwa wakulima baada ya mazao kuuzwa kwenye mnada, akieleza kuwa kuchelewesha malipo kunawavunja moyo wakulima na kudhoofisha mfumo wa ushirika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Ndg. Alfred Francis, ametoa maelekezo kwa viongozi wa vyama vya msingi kufanya ukaguzi makini wa korosho zinazoletwa na wakulima na kuhakikisha kiwango cha unyevu hakizidi asilimia 10 ili kudumisha ubora unaokubalika.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa ilijumuisha pia ukaguzi katika ghala la Maranje linalomilikiwa na Bodi ya Korosho Tanzania, pamoja na ghala la Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU), ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha uendeshaji wa biashara ya korosho katika mkoa wa Mtwara.