Latest Posts

SERIKALI YATAHADHARISHA NGOS KUHUSU UTAKATISHAJI FEDHA KIPINDI CHA UCHAGUZI

Serikali imeonya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na Asasi Za Kiraia (AZAKI) kutokubali kutumika kama njia ya kutakatisha fedha kwa maslahi ya watu binafsi au vikundi mbalimbali, ikiwemo vya kisiasa, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka huu wa 2025.

Onyo hilo limetolewa Jumatatu Agosti 11, 2025, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis, wakati akifungua Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo Dkt. Dorothy Gwajima.

Mwanaidi amesema kuwa mashirika hayo yanapaswa kuwa na uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu, kwani ndiyo msingi wa kutambuliwa kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa.

“Ni muhimu kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuzingatia misingi ya maadili, sheria na kanuni. Tusikubali kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi au vyama vya siasa, hasa katika mwaka huu wa uchaguzi,” amesisitiza.

Kwa upande wao baadhi ya wawakilishi wa NGOs, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Peace Solution Tanzania, Edward Mwenisongole, wameunga mkono wito huo kwa kusema kuwa ni wajibu wa mashirika hayo kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya vitendo vya utakatishaji fedha, kwani vinaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi.

Kongamano hilo la mwaka 2025 linafanyika kwa kaulimbiu isemayo: “Tathmini ya Miaka Mitano kuhusu Mchango wa NGOs katika Maendeleo ya Taifa: Mafanikio, Changamoto, Fursa na Matarajio.”

Lengo kuu la kongamano hilo ni kufanya tathmini ya mchango wa mashirika hayo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, pamoja na kuangazia changamoto, fursa zilizopo na matarajio ya siku zijazo kwa ajili ya kuimarisha ushiriki wa sekta hiyo katika maendeleo ya taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!