Latest Posts

SERUKAMBA AOMBA RADHI KWA WATUMISHI WA UMMA MKOANI IRINGA

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, ameomba radhi kwa watumishi wa umma aliowakwaza kipindi cha uongozi wake, akisisitiza kuwa hakuwa na nia mbaya bali alitimiza majukumu kwa mujibu wa sheria na maadili ya utumishi wa umma.

Serukamba alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi kwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ambapo alikiri kuwa kulikuwepo na changamoto mbalimbali kwa watumishi, lakini dhamira yake ilikuwa ni kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na uzalendo.

“Naomba msamaha kwa yeyote niliyemkwaza kwa namna yoyote ile. Sikufanya kwa makusudi, bali kwa lengo la kusimamia majukumu kwa ufanisi,” alisema Serukamba.

Akizungumzia sakata la vibanda katika Soko la Mji wa Mafinga, Serukamba alisema kuwa lilikuwa jambo gumu na la muda mrefu ambalo lilisababisha Halmashauri kupoteza mapato kwa miaka mingi kutokana na uendeshaji usio rasmi.

Alifafanua kuwa licha ya vikwazo vingi, alisimama imara katika kuhakikisha mchakato wa kurekebisha hali hiyo unafanikiwa, ikiwa ni pamoja na kupinga majaribio ya kuhongwa ili aachane na mchakato huo.

“Wapo waliokuja kuniomba niache kufuatilia suala hilo, wengine wakitaka kunihonga pesa. Niligoma, kwa sababu nilijua ni haki ya wananchi na halmashauri kupata mapato halali,” alieleza Serukamba.

Kwa upande wake, Mkuu mpya wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alimpongeza Serukamba kwa ujasiri na uzalendo aliouonesha katika kusimamia miradi ya maendeleo, hasa suala la soko la Mafinga ambalo lilikuwa gumzo kwa muda mrefu.

“Serukamba amefanya kazi kubwa. Ujasiri wake katika kushughulikia suala la soko la Mafinga umeiwezesha Halmashauri kuanza kupata mapato halali,” alisema Kheri.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!