Latest Posts

SHAHIDI P9 ADAI KUSHAWISHIWA NA LISSU ‘KUKICHAFUA’

Leo Ijumaa ya Februari 20, 2026 kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu imeendelea kwa Lissu kumuuliza maswali ya dodoso shahidi wa 14 ambae analindwa alipewa jina la P9.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru ambapo jana Alhamis ya Februari 19, 2026 shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali Cuthbert Mbilingi alitoa ushahidi wake.

Shahidi huyo anaeleza kwamba yeye ni Fundi umeme mkazi wa Mbeya na alikuwa fundi umeme wa majumbani na viwandani baada ya kusoma masomo yake VETA (2008-2010)

Anaeleza kuwa mwaka 2024 alikua akifuatia mambo ya kisiasa ambapo alivutiwa na sera za Chama cha CHADEMA akawa anafuatilia kwa karibu mikutano ya CHADEMA, matangazo na hotuba za viongozi wa chama hicho.

Anaeleza kuwa matukio aliyofuatilia na kushiriki ni mengi ikiwemo maandamano ya amani yaliyofanyika Mbeya. Anasema palikuwa na route inatoka Uyole makutano yakiwa Kabwe wengine Isangac stendi kwenda Kabwe wengine wakitokea Airport kwenda Kabwe.

Viongozi katika misafara hiyo wakiwa Lissu akitokea Uyole kwenda Kabwe kwingine ilikua Heche kutokea Isanga kwenda Kabwe na Mbowe kutokea Airport kwenda Kabwe.

Shahidi P9 anasema tarehe 3.4.2025 akiwa nyumbani alikuwa akiperuzi kwenye mtandao kupitia simu yake Samsung 8 Pro akiwa anaangalia vitu mbalimbali akaingia katika akaunti ya Instagram. Anaeleza wakati anafungua aliona video ya Mheshimiwa Lissu kwenye akaunti ambayo ilituma (ambayo ameisahau kidogo) akihutubia na kuhamasisha kutokana na vurugu na maandamano ya kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025.

Ameeleza kuwa alimsikia Lissu akisema atauzuia uchaguzi kwa kufanya vurugu na kuuzuia uchaguzi usifanyike akisema “lazima tukichafue”. Ambapo alihamasika na aliona kuna haja ya kufanya hivo.

Tarehe 4.4.2025 akiwa maeneo ya nyumbani na jamaa zake mbalimbali majirani ambapo huwa wanakutana maeneo hayo wakakutana wakawa wanaendelea kujadili maneno ya Lissu kuwa amesema “tukichafue na tuvuruge uchaguzi tunafanyaje, tunaanzaje.”

Wakati wanaendelea na mjadala kuna jamaa yake alimuomba namba yake ya simu wawe wanaendelea kujadili hilo suala akamwambia sawa wakawa wameachana kila mmoja akaendelea na mambo yake.

Tarehe 5 majira ya asubuhi akiwa nyumbani alipigiwa simu na mtu aliejitambulisha kuwa yeye ni mteja anahitaji huduma ya umeme anahitaji kufungiwa umeme akamuelekeza sehemu alipo waonane akasema sawa.

Akakutana nae na alipofika karibu akajitambulisha kuwa yeye ni Afisa wa Polisi akaonyesha kitambulisho chake cha kazi. baada ya kuonyesha kitambulisho chake akaambiwa yuko chini ya ulinzi atapelekwa polisi kwa kosa la “uchochezi wa kuzuia uchaguzi”. Alipofika kutuo cha polisi akakabidhiwa kituoni akahojiwa, ilikua mida ya mchana kuelekea jioni ndugu zake wakamuwekea dhamana akaambiwa awe anaripoti kituoni kila jumatatu ya wiki

April 22, 2025 alipigiwa simu na mtu aliejitambulisha kama Askari Polisi akimwuambia kuwa anahitajika kituo cha Polisi Mwanjelwa akatoka kuelekea kituoni alipofika akajieleza kuwa alipigiwa simu amefika. Akaingia ofisini akaambiwa ameitwa kwa ajili ya kuhojiwa kama shahidi akahojiwa akaandika maelezo yake na akaambiwa aondoke watamuita wakimhitaji.

Anasema wakati anahojiwa palikuwa na askari wawili ambapo mmoja alikua anamhoji mwingine akiwa anachombeza maswali. Ambapo walimhoji juu ya kuhamasisha kuzuia uchaguzi na wakamuuliza lilianzaje na yeye alianzaje kukaa na wenzao kujadili hilo suala.

Akaeleza kuwa aliona clip kwenye mtandao wa Instagram ya Lissu akiongea akihamasisha kuzuia uchaguzi.

Baada ya hapa shahidi akawa ametamatisha ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali Cuthbert Mbilingi.

 

CROSS EXAMINATION

Leo Lissu alianza maswali ya dodoso kwa kumtaka shahidi kutazama maelezo aliyoandika polisi tarehe 22, April 2025 kisha awaeleze majaji kama maelezo hayo ni yenyewe alikiri ni yenyewe na ambapo Lissu aliwaomba majaji wayapikee kama kielelezo ambapo yalipokelewwa mahakamani na kupewa jina la kielelezo D13.

Baada ya hapa Lissu alianza kuuliza maswali ya dodoso na tumekuwekea sehemu ya maswali hayo ya dodoso kama yalivyoulizwa na kujibiwa na shahidi P9.

 

Lissu: Ulisema unaishi Halmashauri ya jiji la Mbeya kwenye maelezo yako umeandikaje

Shahidi: Imeandikwa Mwakibete.

Lissu: Uliulizwa na Wakili wa serikali unafanya shughuli gani ukasema unafanya kazi fundi umeme Halmashauri ya Mbeya, angalia maelezo yako imeandikwa unafanya kazi gani

Shahidi: Imeandikwa mkulima

Lissu: Kazi ni mkulima hapa unajidai fundi umeme, lugha gongana

Shahidi: Kwani huwezi kuwa mkulima ukawa fundi umeme

Lissu: Umesema maandamano yaliongozwa na Mbowe, Lissu na Heche. Angalia kwenye maelezo yako kama Mheshimiwa John Heche yupo kwenye hayo maelezo yako

Shahidi: Kielelezo ni Mnyika sio Heche

Lissu: Jana ulisema Heche

Shahidi: Nilisema Mnyika labda alieandika

Lissu: Umesema ulikuwa nyumbani kwako unaperuzi mitandao kupitia simu yako Samsung 8 Pro

Shahidi: Nilisema Samsung Pro

Lissu: Angalia kwenye maelezo yako kama kuna mahali popote ambapo umesema ulikuwa unaangalia mitandao kupitia sm yako aina ya Sansung Pro

Shahidi: Kama hakuandika ni mwandishi yeye, hayajaandikwa

Lissu: Umesema wakati unaingia Instagram uliona video ya Lissu ila unasema huo mtandao wa Instagram umesahau. Angalia maelezo yako kama ulisema ni akaunti ya nani

Shahidi: Wakili ndio alinihoji hivyo we unatakiwa unihoji nilichoandika.

 

Lissu: Yaani wewe  ndo unaniambia nikuhoji nini

Shahidi:

Lissu: Kwenye maelezo yako ulisema hivi “alisema lazima tukichafue”

Shahidi: Ulisema tukichafue na tukinukishe

Lissu: Nionyeshe kama yapo

Shahidi: Hayapo

Lissu: Ulisema ulihojiwa na mtu mmoja na mwingine alikua anachangia kwa kuuliza maswali mbalimbali, waeleze Majaji kama haya maneno yapo

Shahidi: Hayapo

Lissu: Ulisema uliona clip ya Tundu Lissu ndipo ukaanza(kuhamasisha kuzuia uchaguzi)

Shahidi: Nilisema Polisi mwandishi hakuandika

Lissu: Nataka tumalizane hapa ukawaeleze mapolisi kule hakufai

Shahidi: Watakuwa wanakusikia

Lissu: Hayo maneno kama wewe ni mwanachama wa CHADEMA yameandikwa kwneiye maelezo yako kweli si kweli

Shahidi: Yapo

Lissu: Kwa hiyo mapolisi wamekuingiza chaka

Shahidi: sikuandika maelezo

Lissu: Sasa waambie Majaji kama wewe ni mwanachama wa CHADEMA au si mwanachama

Shahidi: Mimi si mwanachama

Lissu: Ulisema kwamba mfuasi wa CHADEMA, wafuasi wa chadema wana utambulisho gani

Shahidi: Hawana utambulisho

Lissu: Waeleze Majaji umesema hujajiandikisha kokote kama mfuasi hakuna utambulisho wowote waeleze Majaji wataaminije kama wewe ni mfuasi. k

Shahidi: Mimi ni mfuasi kwenye sualaa la kuamini wataamini wao wenyewe

Lissu: Umesema wewe umesoma VETA waeleze Majaji kama umewasilisha vyeti vya kuhitimu mafunzo ya ufundi umeme

Shahidi: Sijawasilisha

Lissu: Umesajiliwa kama fundi umeme

Shahidi: Nimesajiliwa

Lissu: Na nani

Shahidi: Chama cha Mafundi umeme

Lissu: Tarehe 4 April mwaka jana umesema ulikuwa na jamaa zako mnajadiliana kukichafua. Umewataja?

Shahidi: Sijawataja

Lissu: Umesema jamaa yangu mmoja ambae humfaham alikuomba namba, waeleze Majaji mtu ambae humfahamu anawezaje kuwa jama yakk

Shahidi: Simfaham kwa majina

Lissu: Kwa vile unafanya kazi ya ufundi umeme kwa malipo una leseni ya biashara

Shahidi: Sina leseni kwa sababu sina ofisi

Lissu: Una TIN namba

Shahidi: ndio

Lissu: Waeleze Majaji kama kwneye maelezo yako umeitaja

Shahidi: Sikuandika kwa sababu haikuhitajika

Lissu: Waeleze Majaj kitambulisho alichokuonyesha(alionyeshwa na askari) kilikuonyesha ni nani

Shahidi: Nakumbuka niliona jina Vincent na P kama sikosei

Lissu: Waeleze Majaji kama hilo jina lipo kwenye maandishi

Shahidi: Halipo

Lissu: Waeleze majaji tuhuma dhidi yako ya uchochezi wa kuzuia uchaguzi iliishia wapi

Shahidi: Sijajua

Lissu: Waeleze Majaji kama umepelekwa Mahakamani kwa tuhuma ya uchochezi wa kuzuia uchaguzi

Shahidi: Sijawahi kupelekwa

Lissu: Waeleze Majaji kama ulipoitwa Polisi tarehe 22, 4 ulielezwa jambo lolote kuhusu tuhuma za kuzuia uchaguzi

Shahidi: Nilielezwa

Lissu: Waeleze Majaji kama karatasi imeandikwa

Shahidi: Nilieleza ila haikuandikwa

Lissu: Badala yake wamesema hiyo tarehe walikuita kukuhoji kama shahidi

Shahidi: Kweli

Lissu: Ni shahidi kwenye kesi yangu ndio maana umekuja kutoa ushahidi jana na leo

Shahidi: Kweli

Lissu: Waeleze Majaji kama hakuna kosa linaloitwa kuzuia uchaguzi

Shahidi: Najua

Lissu: Unajua kwamba kuzuia uchaguzi ni kosa

Shahidi: Najua

Lissu: Waeleze Majaji kama unajua ni kosa kwa kutumia sheria gani

Shahidi: Mimi si Mwanasheria

Lissu: Ni sheria gani

Shahidi: Mimi si Mwanasheria

Lissu: Kama hufahamu unasemaje kama ni kosa

Shahidi: Kwa upande wa sheria sifahamu ila najua kama ni kosa kuzuia uchaguzi kwa kufanya vurugu. Ukifanya vurugu si kosa?

Lissu: Kwani mimi nimeshtakiwa kwa kufanya vurugu ya uchaguzi

Shahidi: Umeshtakiwa kwa uhaini

Lissu: Kuna viongozi ama wafuasi wowote wa CHADEMA wanajua kama umekuja huku

Shahidi: Nahisi baadhi wanajua

Lissu: Je ulitishiwa na mtu yoyote

Shahidi: Ndio nilitishiwa nikaambiwa lolote baya litanitokea endapo nikitoa ushahidi

Lissu: Waeleze majaji waliokutishia ni akina nani

Shahidi: Siwezi kuwataja

Lissu: Waeleze majaji kama ulitoa taarifa kituo cha Polisi

Shahidi: Ndio nilitoa taarifa

 

Lissu: Kipi

Shahidi: Nikitoa taarifa si bado itajulikana

Lissu: Kituo gani

Shahidi: Nilitoa taarifa kituo cha Polisi Ilomba

Lissu: Ulipewa RB

Shahidi: Ndio

Lissu: Umeiwasilisha mahakamani

Shahidi: Hapana

Lissu: Polisi uliowaeleza hiyo taarifa walichukua hatua gani

Shahidi: Walisema watafuatilia

Lissu: Waeleze majaji kma kuna mtu amekamatwa au kupelekwa mahakamani

Shahidi: Hamna

 

Lissu alitamatisha kuuliza maswali ya dodoso ambapo upande wa Jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga uliuliza maswali ya ziada akitakiwa kufafanua juu ya tofauti kati ya eneo la Mwakibete na Halmashauri ya jiji la Mbeya. Shahidi aliieleza Mahakama kuwa Mwakibete ni Kata ambayo ipo Halmashauri ya Jiji la Mbeya

 

Shahidi alitakiwa kufafanua juu ya kazi yake ambapo anaeleza kuwa awali mpaka mwaka 2008 alikuwa analima na kuanzia mwaka 2008-2010 alienda kusomea ufundi umeme

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!