Wazazi, walezi pamoja na wadau wengine wa elimu wametakiwa kuchukua nafasi yao kikamilifu katika kuimarisha ujifunzaji wa watoto wakiwa majumbani, hususani katika stadi za msingi za kusoma, kuandika na kuhesabu, ili kuongeza ufanisi wa elimu ya awali na msingi.
Hayo yameelezwa Januari 19,2026 Mkoani Kilimanjaro na Mkurugenzi Mtendaji wa Uwezo Tanzania Baraka Mgohamwende katika Mkutano uliokutanisha Taasisi tatu za Uwezo Tanzania,Uwezo Uganda na Usawa Agenda kutoka Kenya kwa lengo la kujadili ajenda ya kikanda ya mageuzi ya ujifunzaji wa Msingi kutoka Muungano wa Foundation Learning Assessments for a Regional Agenda (FLARA).
“Mpaka sasa tumeweza kuwa na tathimini iliyomuangazia mtoto akiwa nyumbani kwake na siyo shuleni kwa nchi za Afrika Mashariki walizo fanyia utafiti mwaka jana inaonesha kuwa kati ya watoto 10 watoto 4 ndio wenye umahiri wa kuweza kusoma angalau aya moja na kufanya hesabu rahisi hivyo bado juhudi zinahitajika katika kuangazia hali halisi” alisema Mgohamwende.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Uwezo Uganda Dkt.Gorrette Nakabugo ameeleza kuwa takwimu wanazozalisha siyo kwa Serikali pekee yake bali na kwa wazazi kwani uwezo wa watoto kujifunza ni shirikishi kwa wadau wote huku akisisitiza wazazi wanapaswa kufahamu hatua zote muhimu kwa watoto kufahamu kuhesabu,kusoma na kuandika hata wanapo rejea kutoka shule.
Naye amesema kuwa katika Nchi tatu za Afrika Mashariki watalinganisha Nchi inayofanya vizuri kuliko nyingine ili kupata maarifa ya kufahamu wameweza vipi kuwezesha watoto kufahamu kusoma,kuhesabu na kuandika.
Wawakilishi kutoka wizara husika za kitaifa za Uganda,Kenya na Tanzania wameshiriki katika Mkutano huo ili kuhakikisha tathimini zinaendana na mifumo ya mitaala inayozingatia umahiri na mipango ya kimkakati ya sekta ya elimu, ambapo kufikia mwaka 2030 FLARA inalenga kutoa angalau tathimini mbili za kitaifa zinazoongozwa na Wananchi na zilizoainishwa katika kila Nchi,pamoja na kuchapisha angalau ripoti mbili za kikanda.
