Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Mara limetumia Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao huharibu mazingira.
Akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Mara, Bi Joyce William, alisema majiko ya umeme yanayopendekezwa na shirika hilo yanatumia kiasi kidogo cha umeme na hivyo ni nafuu kwa matumizi ya kaya.
“Majiko haya yanatumia umeme kidogo sana. Kwa mfano, kilo moja ya nyama inapikwa kwa kutumia unit 0.9 sawa na shilingi 321. Hii inaondoa hofu ya wananchi kuhusu gharama na kuthibitisha kuwa ni nishati nafuu zaidi kulinganisha na zingine,” alisema Joyce.
Aidha, Joyce aliongeza kuwa TANESCO imejipanga kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa akisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kulinda mazingira na kupunguza gharama kwa wananchi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndg. Ismail Ali Ussi, aliipongeza TANESCO kwa ubunifu na juhudi zake katika kutoa elimu, akibainisha kuwa elimu hiyo itasaidia kubadili mitazamo ya wananchi kutoka matumizi ya kuni na mkaa kwenda kwenye nishati safi.
“Tunapongeza TANESCO kwa kuendelea kuwa wabunifu na kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia. Hatua hii inalinda mazingira na afya ya jamii,” alisema Ussi.
Elimu hiyo imepewa nafasi katika mbio hizo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kupunguza changamoto za kiafya na kimazingira zinazotokana na matumizi ya nishati duni.