Latest Posts

TANESCO TARIME: UTAFITI WA KAYA ZISIZO NA UMEME SIYO KAMPENI

Na Helena Magabe, Tarime.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Tarime, Mhandisi Masimino Swalo, amewataka wananchi kutambua kuwa utafiti unaoendelea wa kutambua kaya zisizo na umeme si sehemu ya kampeni za uchaguzi, bali ni utekelezaji wa mpango wa Energy Compact (M300) uliozinduliwa Januari 2025.

Akizungumza na Jambo TV, Swalo alisema mpango huo ulitokana na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliofanyika Tanzania Januari 27-28, 2025, ambapo viongozi walibaini kuwa zaidi ya kaya milioni 300 barani Afrika hazina umeme. Lengo la mkutano huo lilikuwa kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 kila kaya barani Afrika inakuwa imepatiwa umeme wa uhakika, nafuu na endelevu.

“Tunaendelea na utafiti kubaini kaya ambazo hazina umeme. Watu wakituona wasidhani ni kampeni. Huu ni mwendelezo wa Mission 300. Tunataka kila kaya ipate umeme. Tukikuta mtu ameweka hata msingi tu kwenye kiwanja chake, tunaweka nguzo. Pia tutaboresha miradi tuliyoikuta na kukamilisha ile ya REA ilipoishia,” alisema Swalo.

Kwa mujibu wa Swalo, nchini Tanzania bado kaya 8.3 milioni hazijafikiwa na nishati ya umeme, na malengo ni kuhakikisha kila kaya inakuwa na umeme ifikapo mwaka 2030. Alisema kwa kila mwaka wanapaswa kufikia kaya angalau 1,700. Katika Wilaya ya Tarime, utafiti huo ulianza Julai 2025 na tayari kata tano za Tarime Mjini zimekamilika, zikisalia kata tatu kabla ya kuhamia vijijini.

Mbali na hilo, Swalo alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kusisitiza matumizi ya nishati safi. Alibainisha kuwa TANESCO inapanga kuingia ubia na makampuni makubwa, ikiwemo kutoka Uingereza, ili kuzalisha majiko ya umeme yanayotumia nishati ndogo, yatakayosaidia wananchi kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kulinda mazingira.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!