Latest Posts

TEF YALAANI UTEKAJI, YALITAKA JESHI LA POLISI WACHUNGUZE ALIPO POLEPOLE

 

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limetoa tamko rasmi likilaani vikali taarifa za kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, na kulitaka Jeshi la Polisi kuchunguza kwa haraka tukio hilo na kueleza ukweli kwa umma.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Jumanne Oktoba 07, 2025 na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, jukwaa hilo limesema limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa zilizoanza kusambaa tangu Oktoba 6, 2025, zikidai kuwa Polepole ametekwa akiwa eneo la Ununio, Dar es Salaam.

Balile amesema tukio hilo linawakumbusha Watanzania visa vya awali vya utekaji wa watu mbalimbali, akiwemo Mdude Nyagali, Deusdedit Soka, na matukio ya mauaji kama lile la Mzee Ali Kibao.

Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime, limethibitisha kupokea taarifa za kutekwa kwa Polepole na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea.

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amenukuliwa akisema anahoji lini Polepole alirejea nchini, kwani amekuwa akijitambulisha kuwa yuko nje ya nchi.

TEF imesisitiza kuwa uhai na usalama wa Watanzania ni kipaumbele cha kwanza kwa taifa, ikiongeza kuwa amani ya kweli hupatikana pale haki inapodumishwa. “Tunajiuliza, tabia hizi zimetoka wapi? Nani anafanya utekaji huu, na kwa nini?” imeuliza sehemu ya taarifa hiyo.

Jukwaa hilo limeendelea kusisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani, umoja, upendo na mshikamano, hivyo matukio ya aina hiyo hayapaswi kuvuruga taswira hiyo. TEF imelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu ya wazi kwa umma kuhusu nini kimetokea na nani mhusika.

“Utekaji haukubaliki Tanzania,” imesisitiza TEF katika tamko hilo

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!