Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa pongezi kwa Dk. Kaanaeli Kaale kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).
Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa Juni 29, 2025, na kusainiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, jukwaa hilo limesema uchaguzi huo ni ushuhuda wa imani kubwa waliyonayo wanahabari wanawake kwa Dk. Kaale, kutokana na mchango wake thabiti katika tasnia ya habari.
“TEF inaamini kuwa chini ya uongozi wa Dk. Kaale, TAMWA itaendelea kuwa sauti imara ya kupigania usawa wa kijinsia, haki za wanawake na ustawi wa wanahabari nchini,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, TEF imeahidi kuendeleza ushirikiano na TAMWA katika masuala yanayohusu maendeleo ya wanahabari, huku ikimtakia kila la heri Dk. Kaale katika majukumu yake mapya ya kiuongozi.
Pongezi pia zimetolewa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa TAMWA aliyemaliza muda wake, Joyce Shebe, kwa mchango wake mkubwa uliosaidia kuipeleka taasisi hiyo katika hatua za mafanikio makubwa.
“Mungu aendelee kuijaalia kila la heri tasnia ya habari nchini,” ilisomeka hitimisho la taarifa hiyo.