Na Josea Sinkala, Mbeya.
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mkoa wa Mbeya kimeitaka Serikali kutoa msaada wa kisheria kwa weledi kwa wananchi ili kuhakikisha haki inatendeka katika jamii.
Hayo yameelezwa kwenye kilele cha maadhimisho ya Wiki ya sheria Tanzania ambayo kwa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya, maadhimisho hayo yamefanyika jijini Mbeya Februari 03, 2025.
Kupitia maadhimisho hayo, TLS kupitia mwenyekiti wake Kanda ya Mbeya wakili Baraka Mbwilo, ameitaka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya na Serikali kwa ujumla kuhakikisha wanatoa msaada wa kisheria kwa wananchi ili kupunguza kesi katika jamii huku akiomba pia kuongeza mabaraza ya ardhi kutokana na mashauri ya ardhi kuwa mengi nchini.
Wakili Baraka Mbwilo, ameeleza pia kero mbalimbali zinazoikabili sekta ya mahakama hasa wananchi wanapokwenda kufungua mashauri mahakamani akidai gharama ni kubwa hivyo watu wenye ufukara kukosa haki stahiki.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Joachim Tiganga, ameeleza kuwa Mahakama kupitia wadau wake mbalimbali imejipanga kutoa msaada wa kisheria kwa usawa kwa kuwashirikisha pia wananchi juu ya masuala mbalimbali yanayofanywa na Mahakama hiyo.
Jaji Mfawidhi huyo amewataka wananchi kuendelea kuishi kwa kufuata sheria ili kuepukana na mkono wa sheria badala yake wajikite kufanya kazi ili kuendesha maisha yao na kujenga Taifa lao ili kufikia maendeleo endelevu.
Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Zubery Homera aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa ambaye amewataka wadau wa Mahakama wakiwemo watoa msaada wa kisheria kwa jamii kutumia nafasi walizonazo kuelimisha wananchi kujua masuala ya sheria ili pia kuzifikia mahakama kwa urahisi na kupata huduma za kimahakama.
DC Malisa amesema mhimili wa mahakama ndio chombo pekee cha kutafsiri sheria hivyo ni muhimu kuendelea kuheshimiwa na kufanya kazi kwa weledi na uadilifu katika kutoa haki kwa jamii.