Latest Posts

UTAMBUZI WA MIFUGO KUVUKA MIPAKA KIBIASHARA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji, amewataka wafugaji wa Mkoa wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo ili kuongeza thamani ya mifugo yao na kuiwezesha kufikia masoko ya kimataifa.

Dkt. Kijaji ametoa wito huo Julai 10, 2025, wakati akizindua rasmi zoezi hilo kimkoa katika kijiji cha Kambara, wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, ambapo amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imetoa zaidi ya shilingi bilioni 216 kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la kitaifa la utambuzi na chanjo ya mifugo.

Amesema moja ya sababu kubwa inayosababisha mifugo ya Tanzania kushindwa kufikia masoko ya nje ni kukosa utambulisho wa mifugo hiyo, jambo linalowapunguzia wafugaji fursa za kiuchumi.

“Wafugaji wakijitokeza kwa wingi katika zoezi hili, tutakuwa tumefungua milango ya usafirishaji wa mifugo na mazao yake kwenda kwenye soko la kimataifa, lakini pia tutapunguza migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwa kila mfugaji atakuwa na utambuzi wa mifugo yake,”  Kijaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Kighoma Malima, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Maulid Dotto , amesema mkoa wa Morogoro una mifugo zaidi ya ng’ombe milioni 19, mbuzi milioni 17 na kuku milioni 40, na kwamba mifugo hiyo yote inatarajiwa kufikiwa na huduma ya chanjo na utambuzi.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Benezeth Lutega Malinda, amesema chanjo hiyo inalenga kulinda afya ya mifugo na kuzuia magonjwa sugu kama vile homa ya mapafu.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafugaji nchini, Mathayo Daniel, amesema kuwa zoezi hilo ni fursa kubwa kwa wafugaji ambao kwa muda mrefu wamekumbwa na changamoto ya kutoweza kuuza mazao ya mifugo yao kimataifa kutokana na kukosa utambuzi rasmi.

Amesema kuwa kwa sasa kuna matumaini makubwa ya kupata mafanikio ya kiuchumi kupitia sekta ya mifugo endapo wafugaji watajitokeza na kushiriki kikamilifu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!