Serikali imetoa wito kwa vijana nchini kuhakikisha wanalinda amani ya Taifa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo endelevu.
Akizungumza Jumanne, Agosti 12, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus, amesema vijana wana nafasi kubwa ya kudumisha mshikamano wa kitaifa kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Kwa kaulimbiu ya mwaka huu “Nguvu Kazi ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu”, Zuhura amewahimiza vijana kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kujifunza, kubuni, na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa ubunifu na maarifa.
Ameeleza kuwa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 (Toleo la 2024) inaweka mkazo katika kukuza vipaji, uvumbuzi na ubunifu ili kuwawezesha vijana kushiriki ipasavyo kwenye maendeleo ya Taifa.
Maadhimisho hayo yamewakutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakisisitiza umuhimu wa mchango wao katika maendeleo bila kuhatarisha amani na mshikamano wa kitaifa.