Viongozi wawili (2) wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliokuwa wamekamatwa kwa nyakati tofauti na kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa siku kadhaa, hatimaye leo Jumanne Julai 15.2025 wameachiwa kwa dhamana na Jeshi hilo.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mambo ya Nje na Diaspora, John Kitoka imeeleza kuwa viongozi hao ambao ni Brenda Rupia (Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi) na Leonard Magere (Mtaalamu wa Rasilimali, Miradi na Uwekezaji) kila mmoja ameachiwa kwa dhamana yenye masharti ya kutakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Kati (Central Police Station), Dar es Salaam kesho, Jumatano ya Julai 16.2025
Wawili hao walikamatwa kwa nyakati tofauti Julai 12.2025, ambapo Brenda alikamatwa akiwa katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Namanga akielekea nchini Kenya na baadaye alitarajiwa kusafiri kuelekea nchini Ujerumani kwa ziara ya kikazi.
Magere yeye alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) akielekea nchini Uingereza kwa ziara ya kikazi
Licha ya kwamba viongozi hao wamepatiwa dhamana, lakini chama hicho kimesema kinaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa jambo hilo, huku kikisitiza uwepo wa haki, usawa na kufuatwa kwa taratibu katika mchakato mzima
Hata hivyo, CHADEMA imetoa shukrani zake kwa wafuasi wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla wake kwa namna wanavyoshikamana na kuwaunga mkono katika nyakati hizi ngumu wanazopitia.