Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini na Madhehebu mbalimbali Mkoa wa Dar es Salaam imewataka viongozi wa dini nchini kubaki katika nafasi zao za kiroho na kuepuka kushiriki au kutoa kauli zinazoweza kuchochea uvunjifu wa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza katika Kongamano la Kamati hiyo lililofanyika Aprili 23, 2025 katika Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad, aliwaonya baadhi ya viongozi wa dini wanaotoa matamko ya kuishurutisha serikali badala ya kushauri kwa hekima.
“Viongozi wa dini tuzijue nafasi zetu. Mtu wa siasa mwache afanye kazi ya siasa. Bahasha zisikutoe katika nafasi yako,” alisema Sheikh Walid huku akiikumbusha jamii kuwa serikali ni mamlaka iliyowekwa na Mungu, hivyo inapaswa kuheshimiwa.
Sheikh Walid pia alionya matumizi mabaya ya vipaza sauti katika nyumba za ibada, akisema vinaweza kuwa hatari zaidi ya bunduki endapo vitatumika kueneza chuki.
“Siyo kila mtu anayekuja katika nyumba ya ibada unataka kumpa kipaza sauti. Kabla hujasema neno, fikiria kwanza – neno likitoka halirudi,” alisisitiza.
Katika kongamano hilo, viongozi wengine wa dini walieleza maoni yao kuhusu nafasi ya taasisi za kidini katika kulinda amani ya Taifa:
Askofu Allen Siso, Katibu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, alisisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho la matatizo yanayowakabili wananchi.
“Tuwe sehemu ya kutoa majibu kwa wanachosumbuka nacho watu. Viongozi wa serikali waje kwetu kupata suluhisho,” alisema.
Askofu Dk. Sylvester Gamanywa, Mwangalizi wa Wapo Mission, alisisitiza umuhimu wa kutumia “soft power” au nguvu ya ushawishi badala ya mabavu katika kuzuia uasi wa kisiasa.
Kwa upande wake, Mama Shamim Khan, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) na mjumbe wa Kamati hiyo, aliwataka wananchi kutii viongozi waliopo madarakani huku akiwakumbusha kuwa mamlaka yao yanatambulika pia na vitabu vitakatifu.
“Tukemeane. Kuna watu wanatoa lugha chafu dhidi ya Rais. Viongozi wa dini mnapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea ili kulinda amani ya nchi,” alisema Mama Shamim ambaye pia aliwahi kuwa Waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu.
Sheikh Mharram Mziwanda naye alionya dhidi ya tabia ya viongozi wa dini kuishurutisha serikali badala ya kutoa ushauri wa kujenga kwa maslahi ya taifa.
Kongamano hilo liliwakutanisha viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali mkoani Dar es Salaam, likilenga kujadili nafasi ya taasisi za kidini katika kulinda na kutetea amani ya nchi kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025–2030.