Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Denis Londo, ametaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuendelea kusimamia amani, usalama wa raia na mali zao, sambamba na kuimarisha mahusiano kati yao, Serikali na wananchi kwa nyakati zote wakati wa shida na raha ili kujenga imani na mshikamano wa kitaifa.
Waziri Londo amesema hayo wakati wa mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, yaliyofanyika ofisini kwa Mkuu huyo wa mkoa, ambapo ameeleza kuwa kazi ya msingi ya viongozi ni kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinatekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa maelekezo ya serikali.

Amesisitiza kuwa vyombo hivyo ni vya wananchi na hivyo ni muhimu kwa wananchi kuona matunda ya kazi na maboresho mbalimbali yanayofanywa na serikali katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema kuwa taasisi za ulinzi na usalama mkoani humo zimekuwa mfano wa kuigwa kwa namna zinavyoimarisha hali ya usalama, na kuongeza kuwa Serikali imeanza kutoa vitendea kazi kama magari kwa taasisi hizo, jambo ambalo limepunguza changamoto za upatikanaji wa huduma hususan katika maeneo ya mbali.
Aidha, Adam Malima ameiomba Wizara hiyo kusaidia ujenzi wa miundombinu ya Magereza katika wilaya za Gairo, Malinyi na Kilosa pamoja na kuboresha majengo ya ofisi, huku akiipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kwa kutoa magari mapya kwa Jeshi la Zimamoto ambayo yameboresha uwezo wake wa kukabiliana na majanga.

Kuhusu idara ya Uhamiaji, Malima amesema imefanikiwa kudhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu, hali iliyosaidia kuimarisha usalama katika mkoa huo.
Amesema, juhudi hizo zimechangia kuwapa wananchi mazingira bora na salama ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii, huku akisisitiza kuwa msingi wa maendeleo ni amani na ushirikiano kati ya serikali, vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi.