Latest Posts

WACHINA WA ‘MABILIONI’ WAPELEKWA GEREZANI, KESI YAO HAINA DHAMANA

Raia wawili (2) wa China ambao ni Weisi Wang (41) na Yao Licong wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya Uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha takribani Shilingi Bilioni Mbili na Milioni Kumi na Tatu za Kitanzania

Washtakiwa hao wamesomewa makosa yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita na Benjamin Muroto mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa Mahakamani hapo leo, Jumatano Januari 07.2026 washtakiwa wote wawili (2) wanakabiliwa na kosa la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, ikielezwa kwamba walitenda kosa hilo tarehe tofauti kati ya Desemba 01.2024 na Desemba 30.2025, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Mwanza na Unguja -Zanzibar, pamoja na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Aidha imeelezwa Mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao kwa makusudi waliandaa genge la uhalifu lililojihusisha na kughushi nyaraka, kunakili kadi za ATM, kukwepa kodi na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu

Katika kosa la pili, washtakiwa wote wanatuhumiwa kutenda utakatishaji fedha, ambapo imeelezwa Mahakamani hapo kwamba katika tarehe hizo hizo za kati ya Desemba 01.2024 hadi Desemba 30.2025, wakiwa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, washtakiwa walijipatia mali ambazo ni Dola za Kimarekani 707,075 pamoja na Shilingi za Kitanzania 281,710,000, huku wakijua wazi kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu wa kuongoza genge la uhalifu

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki alisema kuwa washtakiwa hao hawatakiwa kujibu chochote kwa sasa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo

Pia kwa mujibu wa sheria, mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao hayana dhamana hivyo hawawezi kupata dhamana katika ngazi ya Mahakama hiyo

Upande wa Jamhuri uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa, ambapo kesi imeahirishwa hadi Januari 21.2026.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!