Wajane mkoani Mtwara wameiomba serikali kuwasaidia kuharakisha kesi zao za mirathi pindi zinapofikishwa mahakamani ziweze kufanyiwa mchakato wa haraka ili kuwaepusha na changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Hayo yamebainishwa Juni 23,2025 kwenye maadhimisho ya siku ya wajane duniani ambapo kimkoa yamefanyika ukumbi wa Mustafa Sabodo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara.
Mjane Rahma Ismail amekili kucheleweshwa kwa mashauri ya kesi pindi kesi zinapofika mahakamani hali inayopelekea baadhi yao kukata tamaa na kupelekea kukosa haki zao.
Nae Asha Bakari amesema kuwa changamoto ya kughairishwa kesi na kupangiwa tarehe nyingi kwa muda mrefu inasababisha wajane hao kukosa haki zao za msingi kutokana na kutoweza kumudu gharama za ufuatiliaji wa kesi kama vile nauli ya kufika mahakamani.
Akielezea sheria za mirathi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Mtwara John Marere amesema zipo kesi mbalimbali zinazowakabili wajane hao ikiwemo kufukuzwa kwenye nyumba walizo jenga na waume zao na hupelekea wajane hao kukosa msaada na kuhangaika na watoto.
“Familia nyingi zimekua zikiwafukuza wajane wakati wa ugawaji wa mirathi hali inayopelekea wajane wengi kukosa haki zao na hupelekea wao kupata magonjwa ikiwemo sonona na kususiwa watoto bila msaada wowote kutoka upande wa marehemu hivo basi niwaombe wajane wote pindi unapoona mambo hayaeleweki basi wahi haraka katika ofisi za serikali za mitaa au fika katika madawati ya kijinsia tuweze kukusaidia.”Amesema Marere
Aidha Mratibu wa wajane Kanda ya Kusini Cecilia Erio amebainisha changamoto mbalimbali wanazozipitia ikiwemo kunyanyapaliwa na ndugu wa mume na kutuhumiwa kuhusika na vifo vya waume zao pamoja na changamoto ya ugawaji wa mirathi.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rachel Kasanda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amesema takribani wanawake 310 wametelekezwa na wajane 54 wamefanyiwa ukatili wa kimwili hali inayoleta hofu kwa baadhi ya wajane.
Hivyo amewaomba watumie fursa mbalimbali zilizopo kwenye jamii ili ziwawezeshe kuendesha familia zao na kujimudi katika maisha yao pamoja na kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
Hata hivyo Meneja wa Nanauka Foundation Joel Nanauka amewasilisha mada inayohusu mambo yanayowakwamisha wajane kuendelea kiuchumi ikiwa ni pamoja na kukata tamaa ya maisha, kukaa na kuishi na maumivu kwa muda mrefu bila kusamehe pamoja na kukosa ujuzi wa mambo wanayotaka kufanya hivyo ametoa rai kwa wajane hao kujifunza na kujiunga katika vikundi mbalimbali vya wajane vitakavyowawezesha kupiga hatua kiuchumi.