Licha ya kuwapo kwa masoko ya uhakika na fursa mbalimbali za kifedha, wakulima wa zao la mtama katika Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma bado wanakabiliwa na changamoto zinazokwamisha uzalishaji wa zao hilo kwa tija.
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, ukosefu wa mitaji, wadudu waharibifu (Suwenje), na ucheleweshwaji wa mikopo kutoka kwa taasisi za kifedha na mamlaka zinazohusika na utoaji wa mikopo.
Hayo yameelezwa na wadau wa kilimo katika kikao cha Jukwaa la Wadau wa Zao la Mtama, kilicholenga kuimarisha upatikanaji wa masoko na fursa za kifedha kwa wakulima,Kikao hicho kiliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la ActionAid Tanzania kwa kushirikiana na World Food Programme (WFP) na kufadhiliwa na Ubalozi wa Ireland kupitia mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama.
Akizungumza katika kikao hicho, mkulima kutoka Kijiji cha Godegode, Alex Ngombwe, amesema kuwa licha ya kuwa na maeneo makubwa ya kulima, wengi wao wanakosa vitendea kazi na mikopo ya wakati ili kuongeza uzalishaji.
“Inawezekana nina heka 20 au 30 lakini nashindwa kuzitumia kikamilifu kutokana na ukosefu wa zana za kisasa,Tunalazimika kuzunguka kwenye mabenki kuomba mikopo bila mafanikio. Tunaomba serikali na mashirika yatusaidie kupata mikopo kwa wakati ili tuweze kulima kwa tija,” amesema Ngombwe.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Mpwapwa, Daniel Sallah, amesema ucheleweshwaji wa mikopo umekuwa changamoto ya muda mrefu kwa wakulima.
“Tunaomba taasisi za kifedha kama CRDB na NMB zitoe mikopo kwa wakati. Wakulima wamekuwa wakilia kwa muda mrefu kuhusu suala hili,” ameeleza Sallah.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Gideon Bakuza, amewataka wakulima kutunza chakula walicho nacho kwa sasa kutokana na hali mbaya ya hewa inayotarajiwa kuathiri upatikanaji wa mazao.
“Tuna miezi tisa hadi msimu mwingine wa kilimo, hali si nzuri. Bei ya mtama sasa ni Sh 700 lakini inaweza kufika hadi Sh 1,000. Mahindi debe moja ni Sh 26,000. Tuwe makini na tunze chakula tulicho nacho, tusiuze kwa sababu zisizo za msingi,” amesisitiza Bakuza.
Kwa mujibu wa shirika la ActionAid Tanzania, kupitia kwa Mratibu Cosmas Bauleche amesema mradi wa Kilimo Himilivu cha Mtama umefikia zaidi ya wakulima 40,000 mkoani Dodoma, ukiwa na lengo la kuwawezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuongeza tija katika kilimo.
Mradi huu ulianza mwaka 2018/2019 na hadi sasa unatekelezwa katika kata 11 za Wilaya ya Mpwapwa, ukihusisha vijiji 52 na zaidi ya wakulima 9,000 kupitia vikundi 113 vilivyoundwa rasmi.
Manufaa ya mradi huo ni pamoja na kuwajengea wakulima uwezo kupitia mafunzo ya kanuni bora za kilimo, kuwapatia zana za kisasa kama mashine za kupandia na kupuria mtama, pamoja na kuboresha mnyororo wa thamani wa zao hilo.