Latest Posts

WALIA KUCHOMEWA NYUMBA NA KUPIGWA WAKIDAIWA KUVAMIA ENEO LA MWEKEZAJI UVINZA, KIGOMA

Wakazi wa kitongoji cha Tandala, kilichopo kijiji cha Chakuru, kata ya Uvinza, wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma wamelalamikia kufanyiwa vitendo visivyokuwa vya kiungwana na maafisa wanaotajwa kuwa ni wa maliasili ambao kwa muda sasa wamekuwa wakichomewa nyumba zao, kuharibiwa mazao, kupigwa na kufanyiwa matendo mengine yanayovunja haki za binadamu kwa kile kinachodaiwa kuwa wamevamia kwenye eneo hilo ambalo ni la mwekezaji.

Akizungumza na Jambo TV mapema siku ya Jumatatu Juni 10,2024 Katibu wa CCM tawi la Tandala ambaye ni mkazi wa eneo hilo Amos Msonge ameeleza kuwa wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakipitia mateso na manyanyaso makali ambayo kwa muda mrefu yameshindwa kutafutiwa majawabu na viongozi wa serikali na chama tawala (CCM) licha ya jitihada mbalimbali alizozichukuwa yeye binafsi ikiwemo kufika kwenye ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Uvinza na ofisi ya Katibu wa CCM mkoa wa Kigoma ili kutafuta majawabu ya changamoto hiyo.

Amesema eneo hilo wamekuwa wakiishi kihalali kwani walikabidhiwa na serikali mwaka 2018 ambapo zoezi la kuwekwa ‘bikoni’ mpya lilifanyika, lakini vitendo wanavyofanyiwa sasa ikiwemo kuchukuliwa fedha na vitu vyao vingine kwa nguvu vinatengeneza maswali lukuki yanayokosa majibu kwao, na kwamba hadi kufikia Mei 25 mwaka huu zaidi ya kaya 30 zimeathirika na zoezi hilo.

Jambo TV imezungumza kwa njia ya simu na Mkuu wa wilaya ya Uvinza Dinnah Mathamani ambaye amekiri kupokea malalamiko hayo, hata hivyo amesema katika eneo hilo kuna doria inayofanyika kwenye vitalu vya Halmashauri ya wilaya ya Uvinza ili kuhakikisha vitalu hivyo vinakuwa salama kwa ajili ya wawekezaji (wa mifugo), sambamba na hilo iko doria nyingine inayofanyika kwenye kitalu cha uwindaji kinachoanzia Kasulu hadi NARCO ambako kote amesikia malalamiko ya wananchi kufanyiwa ndivyo sivyo.

Katika kushughulikia changamoto hiyo Mathamani amesema juma lililopita ameandika barua na tangazo katika vijiji vyote vinavyozunguka maeneo hayo ili wale wenye mali zao ikiwemo mazao ya vyakula nk, kwenye vitalu au ranchi za Taifa wajaze fomu ili waweze  kuvuna mazao hayo kwa mwezi nzima bila kufanyiwa vurugu yoyote, na kwamba tangazo hilo limesambazwa kwenye vijiji vyote vinavyozunguka eneo hilo la uwekezaji.

Mkuu wa wilaya huyo amekanusha vikali madai ya wananchi kuwa wamemilikishwa eneo hilo badala yake ameeleza kuwa wakati mwingine wananchi hao wamekuwa wakisema uwongo kwa kuwa maeneo hayo yapo rasmi kama ranchi za Taifa (NARCO) na maeneo mengine ni vitalu ambavyo vimekodishwa kwa muindaji kuanzia Kasulu NARCO hadi kuingia maeneo ya Uvinza (yaani eneo hilo kuna upande upo Kasulu na upande mwingine upo Uvinza), na kwamba muindaji huyo ana vibali vya miaka kadhaa.

Ameendelea kufafanua kuwa siku za nyuma serikali kupitia  yeye (Mkuu wa wilaya Uvinza) na Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye walimuita muindaji (mwekezaji) huyo na kumtaka kutofanya vurugu kwa wananchi licha ya kwamba wameingia kinyume na taratibu badala yake awaache wavune mazao yao kwa amani na utulivu.

Aidha, amesema kamati ya kitaifa ya Mawaziri nane (8) ilitolea maelekezo eneo hilo ambapo ilielekeza kuwa NARCO itoe hekta 3500 na Halmashauri itoe hekta 5000 na kufanya jumla ya hekta 8500 ili wakabidhiwe wananchi, jambo ambalo kwa sasa linafanyika na kwamba hadi sasa Kamishna wa Ardhi mkoa wa Kigoma na wataalamu wengine wa Ardhi wapo kwenye maeneo hayo wakitekeleza maagizo hayo.

Vilevile, ameseme zoezi hilo limekuwa endelevu kwa miaka takribani mitatu (3) sasa ambapo kwa mwaka jana (2023) pekee wananchi wote walioathirika kutoka kwenye kaya takribani 740 walitengewa eneo na kupangiwa makazi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!