Na; mwandishi wetu
Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Misisi uliopo kata ya Sazira, Bunda mkoani Mara ambao ni waathirika wa shughuli zilizofanywa na Shirika la CCECC (China Civil Engineering & Construction Company Limited) kutoka nchini China wameandika barua ya malalamiko kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wakieleza kile walichodai kuwa ni dhuluma na uonevu waliofanyiwa na kampuni hiyo
Kupitia barua hiyo ambayo Jambo TV imeiona, wakazi hao wamesema shirika hilo linalohusika na masuala ya ujenzi na kwamba liliingia kufanya kazi kwenye makazi yao kinyume na taratibu mwaka 2020
“Hili ni shirika linalojihusisha na masuala ya ujenzi na hapa lilikuwa linapiga mabaruti kwa ajili ya kuchoronga mawe yaliyokuwa yanachukuliwa kwa ajili ya Lami (yaani kubangua lami) kupelekwa kujengea mradi wa barabara kubwa inayounganisha kule Butiama, kutoka Bunda kwenda Nyamuswa mpaka kule kwa Mwalimu Nyerere, na pale inasemekana ya kwamba Madini ujenzi yaliyopo hapo kwa maana ya mawe yanayorongwa pale yana chembechembe na viashiria vya uwepo wa madini”
Wamedai shirika hilo limeingia kwenye eneo hilo kinyume na taratibu, kwani hakukuwa na mikataba rasmi kwa wakazi wa eneo hilo hasa wale waathirika wa zoezi hilo
Akizungumza na Jambo TV Felix Joseph Maiga ambaye pia ndiye aliyesaini barua iliyotumwa THBUB amesema uharibifu mkubwa wa mazingira umejitokeza katika eneo hilo, lakini shirika husika halikuweza kulipa fadhila kwa namna yoyote ile kwa waathirika
Maiga ambaye kupitia barua iliyotumwa THBUB amejitambulisha kuwa ni Katibu wa Familia za Wahanga na Waathirika wa Shughuli za Kampuni ya CCECC -Bunda, Mara ametaja baadhi ya athari zilizowakumba wakazi wa mtaa huo kuwa ni pamoja na vifo, majeraha, kupooza, kubomoka kwa nyumba za wakazi, bati kutoboka, kukauka kwa vyanzo vya maji na mazao, vumbi kali, kukosekana usikivu kutokana na milipuko, kusababisha maradhi na magonjwa ya vifua, vikohozi, michubuko, mba nk
Kufuatia malalamiko hayo, Jambo TV imemtafuta Diwani wa Kata ya Sazira aliyemaliza muda wake ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Bunda Michael Kweka ambaye amekanusha vikali uwepo wa madai hayo kwa kueleza kuwa waathirika wa mradi huo walishalipwa fidia zao muda mrefu chini ya uratibu wa TANROADS mkoa wa Mara
Katika ufafanuzi wake, Kweka ameenda mbali zaidi na kueleza kuwa wanaoibua jambo hilo kwa sasa wana dhamira ya kuchafua taswira ya chama tawala (CCM) na serikali yake inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan jambo ambalo yeye hatoweza kuvumilia kwani madai hayo hayana uhalisia isipokuwa anaamini ajenda hiyo inaibuliwa na wapinzani wake kisiasa wanaoleta ili kumchafua yeye binafsi, chama chake na serikali jambo ambalo halivumiliki
“Hilo eneo watu walishalipwa fidia, hilo eneo TANROADS mkoa wa Mara ilisimamia wakalipa fidia na wale watu wakaachia hilo eneo, lakini baadaye wathirika wengine wa pembeni baada ya karasha kuanza kazi walipata athari za vumbi, bado TANROADS mkoa wa Mara wakalipa tena mara ya pili” -Kweka