Wakazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mkoani Mtwara wamepongeza kampeni ya Kitaa Kimeitika-TB Inatibika-Chukua Hatua kupitia Kliniki Tembezi inayotoa huduma za uchunguzi wa ugonjwa wa Kifua Kikuu ambayo inafanyika bila malipo.
Ni zaidi ya wananchi 200 ambao wamejitokeza mkoani Mtwara kwaajili ya uchunguzi wa ugonjwa wa Kifua Kikuu, zoezi ambalo limefanyika katika kituo cha mabasi Mkanaledi mkoani hapo huku wananchi wakitoa pongezi kwa utaratibu huo kwakuwa umesaidia kupunguza gharama za kwenda kituo cha afya kwaajili ya kufanya uchunguzi, sambamba na hilo pia wametoa wito kwa wananchi wengine kujitokeza ili kupata huduma hiyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma mkoa wa Mtwara Dkt Michael Koni amesema kuwa kampeni hiyo inalengo la kumsadia mwananchi kupunguza gharama za kufanya uchunguzi ambapo itafanyika kwa siku 14 katika halmashauri zote tisa za mkoa wa Mtwara, huku malengo ni kuwafikia wagonjwa zaidi ya 800.
Kampeni hiyo imeratibiwa na ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini Mtwara.