Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) amejikuta akiingia kwenye mgogoro na wananchi wa eneo la Mecco, Kunduchi Mtongani Dar Es Salaam baada ya wananchi hao kudai eneo lao kuvamiwa na Wakala wa Mabasi Yaendayi Haraka (DART) kwa ajili ya kujenga karakana bila ya kufuata utaratibu.
Wananchi hao wameeleza kuwa mwaka 2022 DART walitoa ramani ya kujenga karakana ya mabasi kwa mradi wa BRT lot 04 ambapo walipanga kujenga karakana eneo la Mbuyuni ambapo wangejenga sehemu eneo la mtaa wa Upendo na upande mwingine wa barabara (Mecco Juu).
Lakini baadae wakala huyo akapita na kuandika namba katika nyumba kwenye eneo ambalo lingetumika na mradi, ambapo waliweka namba katika nyumba ambazo hazipo katika ramani.
Hapa ndipo mvutano na wananchi ulipoanza na mwaka huu (2024) ndipo wananchi walipoamua kufungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi dhidi ya DART kuwa wamevamia eneo lao ambapo wananchi walishinda lakini mahakama ikatoa maelekezo kuwa DART waombe tena kibali kwa Rais ili waweze kuruhusiwa kuendelea na mradi.
Wananchi hao wakakata rufaa kuwa maamuzi ya Jaji kuwataka DART kwenda kuomba kibali kwa Rais hawajaridhishwa nayo bali wanataka wakala huyo atumie eneo ambalo lipo wazi la manispaa pamoja na eneo dogo upande walipo wananchi kwa lengo la kuiepusha serikali na gharama za kulipa fidia kwani eneo la wazi lingekuwa nafuu kwa serikali.
“Mheshimiwa Rais atume tume ya uchunguzi kwa nini wasiweke huku(Mecco) wapeleke karakana waweke upande wa pili(eneo la wazi la manispaa) kwa nini watumie kodi za wananchi vibaya kulipa fidia huku eneo la manispaa ni la wazi halijaendelezwa” Mwananchi Benjamin Samweli
Wananchi hao wamedai wana taarifa fiche kuwa eneo la wazi kuna watendaji wa manispaa wameanza kugawiana na kutumia kwa maslahi binafsi huku wakitaka upande huu wa wananchi uumizwe wai wabaki salama.
Mtendaji Mkuu wa DART Dkt. Athuman Kihamia alipopata wasaa wa kuwaeleza wananchi hao alisema “ama katika eneo ambalo la barabara linalosemwa na wananchi ni kweli lipo lakini ukubwa wake hautoshelezi”
Dkt. Kihamia ameongeza kuwa eneo linalohitajika hekari 38 ambapo kwenye eneo la wazi hazifiki lakini upande wenye makazi(Mecco) zinafika.
Wananchi hao walikuwa na malalamiko juu ya kibali cha DART kutekeleza mradi kwani kibali cha kwanza kilikuwa kimeainisha eneo jingine(upande wa kulia na kushoto mwa barabara)
Majibu ya DART ni kuwa tayari mamlaka hiyo ilishapeleka tangazo kwenye serikali ya mtaa kuwa Rais ameridhia eneo hilo na maeneo mengine yanayoguswa na mradi huo yatwaliwe.
Hata hivyo baada ya kuwasikiliza wananchi hao baadae walikubaliana kuliona eneo la mradi ambapo alizunguka na wananchi wakaweza kukagua.
Baada ya kukagua na kuwaonyesha wananchi eneo litalotumika kwa mradi baadhi ya wananchi walidai kutorudhishwa na maelezo pamoja na maamuzi ya wakala huyo huku wakisisitiza kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutoa uamuzi wa kutaka eneo lililo wazi ndilo litwaliwe kwa ajili ya kujenga karakana