Jumla ya wanawake 180 kutoka Taasisi ya Wanawake na Samia wamehitimu mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha VETA mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha kujitegemea kiuchumi kupitia ujuzi wa vitendo.
Mafunzo hayo yalihusisha fani mbalimbali zikiwemo ushonaji, mapishi, upambaji na udereva, yakilenga kuwaandaa wanawake hao kuanzisha shughuli zao binafsi na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Wakizungumza katika hafla ya mahafali, wahitimu hao walieleza kuwa pamoja na kupata ujuzi wa vitendo, bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji na vifaa vya kazi, hivyo kuiomba serikali kuwasaidia kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
“Tumejifunza mambo mengi yenye manufaa, lakini hatuna pa kuanzia. Tunaomba serikali itupe mkono kupitia mikopo hii ili tuanze kujitegemea,” alisema Alice Sanga mmoja wa wahitimu .
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Iringa,Pasiensi Nyoni alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wanawake kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi kwa kutumia ujuzi badala ya kusubiri ajira rasmi ambazo zimekuwa haba.
“Tunawapongeza wanawake hawa kwa juhudi zao. Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuwainua wanawake kiuchumi. Tunawahimiza watumie maarifa waliyopata kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa,” alisema mkuu huyo wa chuo.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwahakikishia wanawake hao kuwa serikali inaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kupitia halmashauri na kuwasihi kujiunga katika vikundi na kufuata taratibu ili kufikia fursa hizo.
“Serikali ipo kwa ajili yenu. Jiungeni kwenye vikundi, andikeni andiko la mradi, fuateni utaratibu. Hii ni hatua muhimu kuelekea mafanikio yenu,” alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Mahafali hayo yalipambwa na maonyesho ya kazi mbalimbali walizojifunza, ambapo wahitimu walionyesha ubunifu na ustadi katika bidhaa mbalimbali, ishara ya utayari wao kuanza maisha mapya ya kujitegemea.