Njombe
Mratibu wa Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 mkoa wa Njombe Lewis Mnyambwa amewaonya waratibu na wasimamizi wa uchaguzi watakaokiuka taratibu za uchaguzi kwa kuwa uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Ameeleza hayo mara baada ya watendaji wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo kutoka Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Iringa kula kiapo cha utiifu wa maadili ya kazi mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Mhe.Liad Chamshana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi rasmi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Tusikichukulie poa kiapo, ni kifungo kwa wale ambao watakiuka taratibu kwasababu uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu na kuna makosa ambayo msimamizi anaweza kuyafanya kwa makusudi ama kwa uzembe”amesema Mnyambwa
Nao baadhi ya wasimamizi wa Uchaguzi waliokula kiapo akiwemo Samson Meda kutoka jimbo la Njombe mjini pamoja na Nuru Sovela kutoka mkoa wa Iringa wamesema kupitia mafunzo hayo watakwenda kuzingatia kanuni,sheria na miongozo ambapo wamewataka wananchi kujiandaa na uchaguzi ili kupata haki yao ya kikatiba.
Waratibu hao wa Uchaguzi wa mikoa,wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi jimbo,maafisa uchaguzi pamoja na maafisa ununuzi wamekula viapo viwili tofauti ikiwemo utunzaji wa siri na kiapo cha kujitoa kwenye vyama vya siasa.