Serikali imesema kuwa takribani watoto milioni 450 Duniani wana matatizo ya uoni yanayohitaji tiba, na wengi wao hawawezi kuifikia tiba hiyo kutokana na kushindwa kumudu gharama
Kwa mujibu wa taarifa za shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa mtoto mmoja (1) kati ya watoto 1,000 ana ulemavu wa kutokuona.
Mkurugenzi wa huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Patrick Nyembea amesema kila siku, mtoto na kijana mdogo anakosa kujifunza ama kushiriki kwenye shughuli za kijamii kutokana na tatizo la uoni ambalo lingeweza kutibika ama kurekebishika
Ameeleza tafiti zinaonesha kuwa watoto kwenye nchi za uchumi wa chini na wa kati wenye upungufu wa kuona wamo hatarini mara mbili hadi 5 zaidi ya kushindwa kuhudhuria shuleni kutokana na changamoto hizo ikilinganishwa na wenzao wenye uoni mzuri
“Takwimu hapa nchini zinaonesha kuwa mwaka 2023, jumla ya watu milioni 1.6 walihudumiwa kwenye kliniki za huduma za macho ambapo takriban asilimia 42 ya waliopokea huduma walikuwa na umri chini ya miaka 15, kati ya watoto wote waliohudumiwa asilimia 6 walifika wakiwa na ulemavu wa kutokuona” -Nyembea
“Miongoni mwa vyanzo vikubwa vya matatizo ya macho kwa watoto na vijana ni pamoja na mzio (Allergic Conjunctivitis) 24%, upeo mdogo wa macho kuona unaorekebishika kwa miwani (refractive errors) 36%, majeraha kwenye macho 6%; mtoto wa jicho (cataract) 10%, makengeza – (1.5%) makovu kwenye kioo cha jicho (1.1%) na vidonda kwenye vioo vya jicho (1.5%), ugonjwa wa surua, upungufu wa vitamin A (0.2%) na saratani ya macho (Retinoblastoma) 0.3%, sababu hizi zote zinaweza kuepukika au kudhibitiwa endapo tutachukua hatua stahiki mapema” -Nyambea
Aidha, amesema maadhimisho ya siku ya afya ya macho kwa mwaka 2024 yamebeba kauli mbiu isemayo ‘Penda macho yako’ ikiwa inahimiza mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla kuchukua jukumu la kulinda na kuimarisha afya ya macho
Ameeleza serikali imekuwa ikifanya kambi maalum za uchunguzi na matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi ili kuongeza kasi katika kuwahudumia wananchi katika maeneo yao na kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kuzifuata huduma hizo
Pia, ametoa rai kwa jamii kuhakikisha wanalinda watoto na vitu ambavyo vinaweza kuhatarisha afya zao za macho, hiyo inajumuisha muda wanaotumia kwenye runinga, simu pamoja na kompyuta
Aidha, jamii inapaswa kuendelea kuhakikisha watoto wanapata mlo wenye vitamin A za kutosha ambazo zinatokana na vyakula kama karoti, maboga, maini na aina nyingine za vyakula asili ili kulinda afya zao
“Ninawahimiza kina mama wenye watoto wadogo kuhakikisha kuwa wanawapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma ili wapate matone ya vitamini A wakati wote wanapohitajika kufanya hivyo, nj vyema sote kama jamii ikiwemo watoto tuhakikishe kuwa tunatenga muda wa kufanya uchunguzi wa afya zetu za macho na kuhakikisha tunapima angalau mara moja kila mwaka au pale inapoelekezwa na watalaam wa huduma za afya” -Nyambea
“Nitumie fursa hii pia kuelekeza Hospitali zote za rufaa nchini ikiwemo zile za rufaa za mikoa kuhakikisha huduma za upimaji wa macho hasa kwa watoto unafanyika, na tunashirikiana na shule au taasisi nyingine zilizopo kwenye maeneo yetu ili kuweza kuzifikia jamii kwa urahisi zaidi ili kupunguza tatizo hili la uoni” -, Nyambea
Kwa upande wake, Mkurugenzi msaidizi magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka Wizara ya Afya Dkt. Omary Ubuguyu amesema katika maadhimisho hayo ambayo yameeenda sambamba na utoaji huduma ya macho bure ,shule 150 zimefikiwa huku watoto 450,000 wamepatiwa huduma ya uchunguzi wa afya zao za macho
Naye, Afisa mradi Sightsevers Edwin Barongo ametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kuhakikisha wanapata huduma sahihi za macho zinazopatikana Hospitali na si kwingineko.